KUWEPO kwa mashirikiano na mshikamano baina ya wazazi, walezi na walimu wa madrasa kunapelekea urahisi wa watoto kupata elimu iliyo bora kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi alieleza hayo katika salamu zilizotolewa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla katika sherehe ya kuadhimisha Mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika Madrasatul Swifatu Nabawiyyatil – Karima (Msolopa ), Kilimani mjini Zanzibar.
Alisema kuwa hufarijika anapoona wanafunzi wengi waliosoma katika Madrasa hiyo wamefaidika kwa kuwa na elimu na nidhamu kunakosababishwa na umoja na mashirikiano waliyonayo wazazi, walezi pamoja na walimu wa madrasa hiyo.
Alisema suala la kupata elimu ni la lazima kwa kila Muislamu kama kama alivyousia Mtume Muhammad (S.A.W) hivyo ni vyema wazazi na walezi kuongeza juhudi kwa kuwasimamia vijana wao kupata elimu iliyobora ili kuwa na jamii inayomjua mola wao na kujua Dini yao sambamba na kulisaidia taifa kupata maendeleo.
Sambamba na hayo Alhajj Hemed alisisitiza suala la malezi yenye kuzingatia maadili mema kwa watoto jambo ambalo itapelekea kumalizika kwa majanga na vitendo viovu kama vile udhalilishaji, uporaji, wizi, utumiaji wa Dawa za kulevya na vyenginevyo.
Akitoa nasaha kwa waumini waliohudhuria maulid hayo, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Zanzibar Shekh Shaaban Albatashy alisema kuwa kuendelea kuadhimisha Sherehe ya mazazi ya Mtume Muhammad ( S.A.W ) kwa chuo hicho ni kuendelea kumuenzi kiongozi huyo wa umma kwa kufanya mambo mema na kuishi kama alivyoishi Mtume Muhammad.
Alisema kufanya hivyo ni kujikurubisha kwa Allah (S.W) na kudumisha amani, upendo na mshikamano baina yao sambamba na kuendelea kuvirithisha mambo mema vizazi vijavyo kuendelea na utamaduni huo wa kuwakutanisha Waumini kutoka sehemu mbali mbali kila mwaka kwa lengo la kumswalia Mtume Muhamad (S.A.W) huku wakitarajia kupata ujira mwema kesho mbele ya haki.
Madrasatul Swifatu Nabawiyyatil Karima ( Msolopa ) ilianza wiki ya Mtume Muhammad kwa matukio tofauti ikiwemo kuzuru Makaburi ya Mashekh, kufanya usafi maeneo yaliyozunguka Madrasa, uchangiaji wa damu, dua ya kuwaombea viongozi wakuu wa nchi, maonesho ya wanafunzi ya kitaaluma na kumalizika kwa Maulid yaliyokutanisha Madrasa kutoka maeneo mbali mbali ndani na nje ya Zanzibar.