Kundi la watoto ni manusura ya maambukizi ya Corona

NA HUSNA MOHAMMED

WAKATI wa janga la Corona hapa Zanzibar, hasa mwishoni mwa mwezi wa Machi na Aprili baadhi ya wazazi na walezi waliogopa kuwapeleka watoto wao kliniki kwa ajili ya kupata chanjo za kuzuia magonjwa mbalimbali.

Hivyo katika makala haya tutaangalia namna ya muitikio wa jamii hasa walezi na wazazi jinsi ya watoto wao walivyowapeleka vituo vya afya kupata chanjo za kinga ya maradhi mbalimbali.

WAZAZI NA WALEZI WANAZUNGUMZIAJE KUHUSU CORONA

Leluu Khamis Juma, mkaazi wa Fuoni, alisema kuwa mtoto wake wa miezi 11 alimpeleka kituo cha afya kupata chanjo yake ya miezi tisa kipindi cha corona kiliposhamiri hapa Zanzibar.

“Nilimpeleka mtoto wangu mwezi wa Machi mwisho kupata chanjo kwenye kituo cha afya Fuoni, kwa kweli huduma zilikuweko lakini baadhi ya walezi na wazazi waliogopa kuwaleta watoto wao”, alisema.

Alisema kuwa alipofika alifuata miongozo yote ya wataalamu wa afya kama kunawa mikono na kuvaa barakoa, ambapo hakukaa hata foleni alimchomesha mtoto wake na kuondoka.

Nae Hajra Ali Silima, Mkaazi wa Amani, alisema aliogopa kwanza kumpeleka mtoto wake kituo cha afya kupata chanjo yam waka mmoja na nusu, lakini baada ya kusikia hakuna tatizo alikwenda.

“Jirani yangu alienda kumpeleka mwanawe wa miezi mitatu kwenye chanjo kituo cha afya cha Sebleni aliporudi akanambia kama hakuna foleni basin a mimi siku ya pili nikampeleka wa kwangu”, alisema.

Akizungumzia kuhusu muongozo kwenye vituo vya afya alisema hatua iliyochukuliwa na serikali ni nzuri kwa kuwa kumeweza kupunguza maambukizi hasa kwenye vituo vya afya kwa kuwa watu walipimwa kwa kipima joto, kuvaa barakoa na kunawa kwa maji safi au kutumia sanitaiza.

MANESI NA MADAKTARI WA VITUO VYA AFYA WANASEMAJE KIPINDI CHA CORONA

Nesi mmoja wa kituo cha afya Fuoni ambae hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa wastani wa watoto waliofika kutoa chanjo kwa kipindi cha janga la corona kiliposhamiri kilikuwa cha wastani.

“Kwa mfano kama Jumatatu tunapokea wastani wa watoto 50 mpaka 70 wapya na wakuendelea lakini kipindi cha mwezi Machi na Aprili tulipata watoto wapatao 40 hivi lakini kadri siku zinavyoenda mahudhurio yalikuwa mazuri.

Nae nesi mmoja wa kituo cha afya cha Rahaleo, hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa hakupewa idhini ya kufanya hivyo na muajiri wake alisema idadi ya mahudhurio wakati wa janga la corona Zanzibar halikuwa bay asana.

“Wazazi na walezi walichukua tahadhari ya juu sana walitupa ushirikiano wa kutosha, walikuja na kuvaa barakoa zao na sanitaiza zao, waliwapimisha watoto wao na kuondoka”, alisema.

Hata hivyo, alichokiona nesi huyo alisema wazazi na walezi waliamini kuwa kupata chanjo kwa watoto wao kutawanusuru na maambukizi ya corona.

KITENGO CHA HUDUMA ZA CHANJO ZANZIBAR

Mratibu wa Chanjo Zanzibar, Yussuf Haji Makame, akizungumza na makala haya huko ofisini kwake Kidongo chekundu mjini hapa, kuhusiana na mahudhurio ya chanjo katika vituo vya afya alisema zoezi la chanjo liliendelea vyema katika vituo vya afya wakati wa janga la corona.

Mratibu huyo alisema pamoja na kuwepo kwa ugonjwa wa corona wazazi na walezi waliitikia wito wa kuwapeleka watoto wao kupata chanjo mbalimbali zinazowahusu.

“Hapa katikati tulilega kidogo hasa mwezi wa Machi mwisho mripuko wa corona ulipotokea hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, lakini zoezi hilo liliendelea vyema hadi sasa”, alisema.

Alisema kwa kawaida mtoto kuanzia siku moja hadi mwaka mmoja na nusu analazimika kupata chanjo za aina tofauti za kinga dhidi ya maradhi, hata hivyo alisema hadi kufikia umri wa miaka mitano anatakiwa kupimwa ili kujua maendeleo ya ukuaji wake.

Akizungumzia kuhusiana na janga la corona na chanjo za watoto mratibu huyo alisema kuwa kundi la watoto wadogo limeweza kunusurika pakubwa na maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu yaani corona

Mratibu huyo alisema si Zanzibar pekee lakini karibu nchi nyingi zilizopata maambukizi hayo hayakuwagusa watoto.

“Ni kesi chache sana za watoto waliokumbwa na maambukizi ya Corona nah ii nadhani hizi chanjo za watoto zimewasaidia kwa kiasi kikubwa sana kuwanusuru na maambukizi ya corona”, alisema.

Hata kama mama ataugua corona lakini watoto waliweza kunusurika, hizi chanjo zinasaidia sana ingawa hakuna utafiti uliofanyika”, alisema.

Hivyo, aliwataka akinamama na jamii kwa ujumla kutodharau umuhimu wa chanjo na kuwataka kuwapeleka watoto wao kwenye chanjo za kawaida na za kampeni maalumu.

Mratibu huyo alizitaja chanjo hizo kuwa ni pamoja na BCG ya kinga dhidi ya kifua kikuu, polio ambayo inajumuisha magonjwa ya kifaduro, donda koo, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo na kinga dhidi homa ya nimonia.

Alizitaja chanjo nyengine kuwa ni chanjo dhidi ya kuharisha, chanjo ya kinga dhidi ya surua.

Yussuf alisema ipo haja kwa wazazi na walezi kujua umuhimu wa chanjo kwa watoto wao chanjo ambazo zinatolewa bure na serikali hata kama vituo vya afya vya binafsi hupata kutoka serikalini.

Mratibu huyo alisema kwa kiasi kikubwa maradhi mbalimbali yanayowasibu watoto yamepungua jambo ambalo linaonesha dhati jamiii imekuwa ikiunga mkono Serikali kwa hili.

“Lengo ni kuwapata watoto wenye afya njema na ndio maana serikali ikaona umuhimu wa kuwapa chanjo watoto bila malipo ili kuwanusuru na magonjwa mbalimbali”, alisema.

ZANZIBAR YOUTH FORUM

Mkurugenzi wa Zanzibar Youth Forum, Maulid Suleiman, akizungumza na makala haya kuhusiana na ugonjwa wa corona kwa watoto alisema kuwa watoto ni muhimu sana hasa katika kuimarishwa afya zao.

“Ni lazima jamii ijuwe umuhimu wa chanjo kwa watoto kwa kuwa mara nyingi ndio wanaoathirika lakini kupatiwa chanjo hizo na nyengine kunawanusuru na magonjwa mengi”, alisema.

Alisema kwa kuwa watoto ni vijana wa baadae wanatakiwa kujengwa kwa afya njema ili waweze kuepukana na magonjwa hatarishi katika makuuzi yao.

Akizungumzia kuhusiana na corona, Mkurugenzi huyo alisema bado jamii ina wajibu mkubwa wa kuendelea kufuata miongozo ya serikali juu ya kujikinga na corona.

HALI HALISI YA CHANJO ZANZIBAR KWA WATOTO

Mapema Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid, akiwasilisha hotuba ya wizara hiyo kuhusiana na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2020/2021 katika kikao cha baraza la wawakilishi kilichovunjwa hivi karibuni, alisema kuwa jumla ya watoto 38,889wenye umri chini ya mwaka mmoja wamepatiwa chanjo za kukinga maradhi ya kuambukiza (Kifua kikuu, Surua, Homa ya Ini, Homa ya Uti wa mgongo, Donda koo, Kifuduro na Pepopunda).

Alisema kiwango cha chanjo kwa watoto wenye umri huo imefikia asilimia 83.3 ambapo huduma hizo za chanjo zinatolewa katika vituo vyote vya afya vya Unguja na Pemba, vikiwemo vituo vya afya vya binafsi vinavyotoa huduma za afya ya uzazi na mtoto.

“Ni vyema jamii ikajua umuhimu wa chanjo kwa watoto na kuwapeleka watoto wao vituo vya afya na kwa bahati njema sana chanjo hizo zinatolewa bure kabisa, hakuna kituo kinachotakiwa kuuza chanjo”, alisema.

Hivyo alitoa wito kwa jamii hasa akinamama wenye watoto wachanga kuwapeleka watoto wao vituoni jambo ambalo litawakinga na magonjwa mbalimbali hapo baadae.

Kwa mukhtaza huo basi jamii itaona namna gani chanjo inavyosaidia kuwakinga watoto na magonjwa mbalimbali hasa katika makuzi yao.