WASHINGTON,MAREKANI

WABUNGE wa Mississippi nchini Marekani wamepiga kura kuondoa alama ya kibaguzi katika bendera ya jimbo. 

Hatua hiyo ni ishara ya hivi karibuni ya harakati za kupinga ubaguzi wa rangi. 

Gavana wa jimbo kwa tiketi ya Republican,Tate Reeves, alisema kuwa atautia saini mswada huo endapo utapitishwa. 

Bunge litateua jopo maalum litakalobuni bendera mpya na kisha kupigiwa kura na wakaazi wa Mississippi mwezi Novemba. 

Bendera hiyo,awali ilikuwa ikitumiwa na majimbo yaliyokuwa yakiwamiliki watumwa na ambayo yalishindwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1861 hadi 65. 

Mjadala wa kuiondoa alama hiyo ulipata nguvu baada ya kifo cha George Floyd aliyeuawa baada ya kukabwa koo na ofisa wa polisi Minneapolis mwezi uliopita. 

Mississipi lilikuwa jimbo la mwisho kuitumia alama katika bendera yake.