NA NASRA MANZI

SERIKALI ya Zanzibar kupitia Tume ya Utumishi Serikalini imefanikiwa kutoa ajira kwa watumishi 16,675 katika ngazi na sekta  mbali mbali ndani ya kipindi cha September 2011 hadi Juni 2019.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, aliyasema hayo wakati akitoa taarifa  kwa wandishi wa habari juu ya maadhimisho ya siku ya Utumishi wa Umma Zanzibar, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo Mazizini Unguja.

Alisema serikali ilifanikia kutoa ajira hizo katika kisiwa cha Unguja na Pemba ndani ya utawala wa awamu y asana inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

Kutokana na hali hiyo Waziri huyo alisema ni vyema viongozi na Watumishi wa Umma, wakaona umuhimu wa kuweka na kutumia takwimu sahihi, ili kuimarisha ubora wa utekelezaji  majukumu yao ya kila siku, sambamba na kufanya maamuzi yenye ushahidi.

Alisema ni vyema viongozi na watumishi kuhakikisha wanatoa huduma zilizobora kwa umma na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuwa wabunifu katika maeneo yao ya  kazi.