NA MWANDISHI WETU
WATALII 273 wameingia nchini kwa mwezi Juni baada ya sekta hiyo kuanza kurejea kufuatia kupungua kwa maambukizi ya corona na kurejeshwa huduma za usafiri wa anga wa kimataifa kama ilivyokuwa awali.
Hayo yalibainishwa na Mtakwimu Kitengo cha Utalii Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Raya Mohammed Mahfoudh alipokuwa akiwasilisha takwimu za uingiaji wa wageni nchini.
Alisema, idadi hiyo ya wageni imeongezeka ikilinganishwa na wageni 173 walioingia kwa mwezi Mei ambapo asilimia 48.4 ya wageni hao walitoka Ulaya sawa na ongezeko la asilimia 40.4.
Alisema, asilimia 52.0 ya wageni hao walipitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na asilimia 48.0 walipitia bandarini.
Alisema, asilimia 52.4 ya wageni ni wanaume na 47.6 walikuwa wanawake ambapo asilimia 3.3 ya wageni walikuwa chini ya umri wa miaka 15, asilimia 93.8 wenye umri wa miaka 15-64 na asilimia 2.9 ni wenye umri wa kuanzia miaka 65.
“Wageni hao walitegemewa kukaa kwa wastani wa siku nane,” alisema.
Mhadhiri wa Uchumi Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), Dk. Stella Ngoma Hassan, alisema, kurejea kwa sekta ya utalii ni faraja kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar baada ya zuio la karibu miezi minne hali ambayo iliifanya sekta hiyo kuanguka.
Hata hivyo, alisema, hali inaweza kuwa nzuri zaidi baada ya hali kutengemaa nchini Italia, ikizingatiwa ndiyo inayotoa idadi kubwa ya wageni wanaoingia nchini.
“Italia ni miongoni mwa mataifa yaliyokumbwa na maambukizi zaidi ya ‘corona’ duniani, kwa kiasi kikubwa kumeathiri hali ya utalii wetu,” alisema.
Aidha, alisema, hali ya uchumi wa dunia itaendelea kukumbwa na mtikisiko kwa miaka kadhaa baada ya janga hilo na kwamba Zanzibar nayo ni sehemu ya dunia hiyo.
Shirika la Ndege la Qatar tayari limefungua safari kuingia Zanzibar baada ya kupungua kwa ugonjwa wa ‘corona’.