NA ABDI SULEIMAN

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed, amesema serikali itaendelea kuziimarisha kaya masikini nchini, katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mradi wa  TASAF kwa wanakaya kubuni miradi endelevu.

Alisema serikali haitamvumilia mtu atakaetumia fedha za mradi huo kinyume na malengo.

Alisema hayo wakati akizungumza na walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini, kutoka shehia tatu za Kambini, Mchangamdogo na Kinyikani wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba.

Alisema kwa sasa mpango huo unataka kukamilisha malipo kwa walengwa wa kipindi cha kwanza awamu ya tatu, ambapo malipo yao yanatarajiwa kutolewa mwezi wa Julai na Agosti, baadae kupatiwa tena miezi miwili ya Septemba na Oktoba.

“Tumeamua kufanya hivyo baada ya kuona ipo haja ya walengwa kupewa haki zao, kabla ya kuanza kwa kipindi cha pili awamu ya tatu, ambayo itahusisha shehia zote za Unguja na Pemba,”alisema.

 “Katika kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu Zanzibar nzima tulikuwa na shehia 204 zenye kaya 32,248 sawa na watu zaidi ya 200,000, ambapo fedha zaidi ya shilingi bilioni 40 zilitumika kulipwa walengwa,”alisema.

Akizungumzia kipindi cha pili awamu ya tatu, alisema kuna  jumla ya shehia 354 sawa na asilimia 100/- ya walengwa kwa Zanzibar ambao zaidi ya shilingi bilioni 40 zimetengwa.

Aliwashukuru viongozi wakuu wa serikali kwa uamuzi wa wa kuendelea kuwapatia ruzuku walengwa wa mpango huo.

Mratibu wa TASAF Zanzibar, Said Saleh Adam, alisema lengo la mpango huo ni akinamama na watoto ndio sababu wakawa mstari mbele katika mpango huo.

Ofisa Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba, Ali Salim Matta, aliwataka walengwa wa mpango huo kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi kwa vijana watakaopita kukusanya taarifa.

Mratib wa Tasaf Pemba, Musa Said, alisema shehia ya Kambini ina walengwa 249, Mchangamdogo 156 na Kinyikani wapo  240, ambapo tayari Kinyikani imeshapokea kiasi cha shilingi milioni 8, Kambini shilingi milioni 9.2           na Mchangamdogo shilingi milioni 5.5 kwa miezi mwili.

Aidha aliwataka wananchi kuzitumia fedha hizo kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao za maendeleo pamoja na kujiwekea hakiba ili kuwasaidia baadae.

Kwa upande wao walengwa wa mpango huo kutoka shehia hizo, waliipongeza serikali kwa kuendela kuwapatia fedha za ruzuku.