NA MWANDISHI WETU, 

CHAMA cha ADA TADEA kimesema uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kupunguza na kutangaza majimbo mapya au kurudisha idadi ya majimbo kama ilivyokuwa awali hakuna kosa lolote kama baadhi ya vyama vilivyoanza kubeza na kulaumu.

Kimesisitiza kuwa  ZEC ina wajibu wa kutangaza, kuongeza au kupunguza majimbo wakati wowote kwa mujibu wa sheria, kwani  jukumu hilo ni lao kufanya hivyo si kosa wala ukiukaji wa sheria na taratibu.

Hayo yameelezwa jana na Naibu Katibu Mkuu  wa ADA TADEA, Rashid Yussuf Mchenga, aliyesema kuna baadhi ya  vyama vya siasa vimeanza kulalamikia uamuzi huo wa ZEC huku akisema vimekosa nguvu ya hoja pia madai yao yamekosa uzito na mashiko.

Mchenga alisema vyama vya siasa havina haki ya kuipangia ZEC ifanye au isifanye jambo lolote hivyo akawataka viongozi wa vyama vya siasa kutambua wana wajibu wa  kutii na kufuata uamuzi, matakwa na maelekezo ya tume hiyo.

Alisema vyama vya siasa visitegemee huruma au hisani toka ZEC badala yake kila vyama vijiandae vyenyewe kimkakati kushiriki uchaguzi, kupata kura za ushindi toka kwa wananchi, ili kushinda  Udiwani, Uwakilishi, Ubunge na Urais.

“Chama chochote kitakosea kuilaumu ZEC inapofanya maamuzi yake kama ambavyo vyama vinavyopitisha maamuzi yao kikatiba na kikanuni nayo iachwe ifanye  ifanyavyo kwa mujibu  wa sheria na kanuni zake”Alisema