LONDON,UINGEREZA

MKUU wa shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kwamba janga la COVID-19 linaendelea kuwa baya zaidi ulimwenguni kote.

Akizungumza na waandishi wa habari, Tedros alisema hali ya kawaida haitorejea hivi karibuni.

Tedros aliongeza kwamba japo nchi nyingi haswa za barani Ulaya na Asia zilifanikiwa kulidhibiti janga hilo, katika mataifa mengine maambukizi yanazidi kuongezeka na yalichukua njia mbaya.

Bila ya kumtaja yoyote jina, Tedros aliwashutumu viongozi wa kisiasa wanaotoa kauli zinazochanganya kuhusu janga hilo.

Tedros alitoa kauli hiyo wakati idadi ya maambukizi ya virusi vya corona imepindukia watu milioni 13 ulimwenguni, na zaidi ya watu 560,000 wamefariki, huku Marekani ikiendelea kurikodi idadi ya juu ya maambukizi mapya.