JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

JIMBO la Gauteng la kaskazini mashariki mwa Afrika Kusini limekuwa kivotu kikuu cha ugonjwa wa corona nchini humo huku maofisa wa afya wa nchi hiyo wakivunja rikodi ya kuchukua vipimo zaidi ya 50 elfu vya corona kwa siku moja.

Taarifa zinasema kuwa maambukizi ya kirusi cha corona ni mabaya na makubwa mno katika jimbo hilo la Gauteng ikilinganishwa na maeneo mengine yote ya bara la Afrika.

Ingawa watu wa afya wanafanya juhudi mbalimbali, lakini kumekuwa na malalamiko ya kutochukuliwa hatua za kweli za kupambana vilivyo na ugonjwa hatari wa COVID-19 nchini humo.

Wafanyakazi wa afya wa Afrika Kusini walifanyia uchunguzi vipimo 56 elfu vya COVID-19 kwa siku moja na kufikisha idadi ya watu wote waliochukuliwa vipimo vya corona nchini Afrika Kusini kufikia milioni mbili. 

Hadi kufikia sasa watu laki mbili na 50,687 walikuwa wamegunduliwa kukumbwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini Afrika Kusini.

Kati ya hao wagonjwa 3,860 walikuwa wameshafariki dunia na laki moja na 18,232 walipona na kuruhusiwa kurudi nyumbani nchini humo. 

Marekani ndiyo inayoongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa corona na vifo vilivyotokana na ugonjwa huo.

Hadi sasa watu zaidi ya milioni tatu walikuwa wamethibitishwa kukumbwa na COVID-19 nchini Marekani, huku watu 136,839 wakiwa wameshafariki dunia kwa ugonjwa huo nchini Marekani hadi sasa.

Mbali na hayo, uchunguzi wa hivi karibuni unaonesha kuwa, Waafrika miolioni 50 huenda wakatumbukia kwenye lindi la umaskini wa kupindukia kutokana na makali ya janga la corona.

Hayo yalikuwemo kwenye ripoti mpya ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ambayo ilibainisha kuwa, maeneo ya magharibi na katikati mwa Afrika ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na hali mbaya ya uchumi iliyosababishwa na janga la COVID-19.