AFRIKA imejaaliwa kuwa na kila aina ya rasilimali zinazoweza kuwafanya wakaazi wa bara hilo kuwa matajiri zaidi hapa ulimwneguni, lakini mambo yamekuwa kinyume kabisa.

Kwa mujibu taarifa za uchumi za ulimmwengu kila mwaka, Afrika ndiyo inayobeba nchi nyingi zaidi masikini pamoja na kwamba baadhi ya nchi hizo zina wingi wa rasilimali ikilinganishwa na hayo yanayoitwa mataifa tajiri.

Katika maeneo mengi ya Afrika ndiko kunakoshuhudiwa umasikini uliokithiri, ambapo ukichanganua sababu za umasikini huo utakuta zimegawika makundi mawili, kwanza majanga ya kimaumbile na pili uporwaji wa rasilimali hizo nje ya bara la Afrika.

Wakati mwengine inakuwa vikugumu kuzuia majanga ya asili kama vimbunga, mafuriko, ukame na kadhalika kwani majanga hayo yanapotaka kujitokeza hakuna muda wa kujiandaa kukabiliana nayo.

Lakini sababu ya pili ambayo ndiyo kubwa zaidi ya uporwaji wa rasilimali za Afrika na kutoroshwa nje ya bara la Afrika hii inaweza kuzuilika, lakini inahitaji ujasiri na utashi wa kisiasa kwa viongozi wa Afrika.

Kutokana na viongozi wengi wa Afrika kukosa ujasiri kutokana na umasikini wa nchi zao, leo hii bara hili limegeuka kuwa uwanja wa mapambano ambapo nchi za kigeni zinawania rasilimali hizo kwa ajili ya viwanda vyao.

Kilinachoshuhudiwa hivi sasa barani Afrika ni makampuni makubwa ya kigeni yakikwapua utajiri wa nchi za Kiafrika pasi na huruma hata kidogo na matokeo yake ni kuenea kwa umasikini, ujinga na magonjwa.

Kwa bahati mbaya sana nchi za Kiafrika hazina uelewa mkubwa wa kuwatambua wezi rasilimali ambao wengi wao wamejificha kwenye mwamvuli mpana unaouitwa uwekezaji.

Changamoto zilizopo ni kama namna gani ya kuzilinda rasilimali za umma zisiibiwe na mabwenyenye wakubwa wakisaidiana na vibwenyenye vingi na vilivyotapakaa ndani ya serikali na nje ya serikali nyingi za Kiafrika.

Moja ya rasilimali inayoibiwa kila uchao barani Afrika na kutoroshwa nje ya nchi dhahabu ambapo kwa mwaka mmoja maelfu ya tani za mchanga wa dhahabu kusafirishwa Ulaya na sehemu nyengine.

Madini ya dhahabu yenye thamani ya mabilioni ya dola yanatoroshwa kutoka Afrika kila mwaka ambapo njia kubwa inatotumika kupitishia dhahabu hiyo ni eneo la mashariki ya Kati na kuuzwa kwenye masoko ya Ulaya na Marekani.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na shirika la habari la nchini Uingereza la Reuters, nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), uliingiza kati nchi za umoja huo dhahabu yenye thamani ya dola bilioni 15.1 kutoka Afrika mnamo mwaka 2016 pekee. 

Kulingana na uchunguzi wa shirika hilo la Reuters kuanzia mwaka 2006 nchi za Umoja huo ziliingiza tani 446 za dhahabu kutoka nchi mbalimbali barani Afrika. 

Kiwango kikubwa cha dhahabu hiyo hakikuorodheshwa katika bidhaa zinazouzwa nje na nchi za Afrika. Watalamu waliohojiwa na shirika hilo walibainisha kuwa kiasi kikubwa cha madini hayo kinatolewa nje ya Afrika bila ya kutozwa kodi na nchi zinazozalisha madini hayo hazipati kitu.

Kampuni za madini za barani Afrika zimeliambia shirika la Reuters kuwa kampuni hizo haziuzi dhahabu kwa Umoja wa Falme za Kiarabu, jambo ambalo linathibitisha kwamba dhahabu hiyo inaingia katika nchi hizo kwa njia ambayo si rasmi.

Serikali za Ghana, Tanzania na Zambia zimelalamika kwamba dhahabu ya nchi hizo inatoroshwa kwa kiwango kikubwa na magenge ya wahalifu na aghalabu katika muktadha wa madhara makubwa kwa mazingira na afya ya binadamu.

Shughuli za kuchimba dhahabu ambazo hapo awali zilikuwa zinafanywa na wafanyabiashara wadogo katika nchi hizo za Afrika sasa imechukuliwa na makampuni makubwa kutoka nje ya Afrika.

Kwa mfano katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo ni mzalishaji mkubwa wa dhahabu, lakini nchi hiyo inaambulia kiasi kidogo cha fedha zinazotokana na mauzo ya bidhaa hiyo nje ya nchi.

Dhahabu iliyojaa maeneo mbalimbali katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaporwa na vikundi vya waasi wanaotumia siala za moto kupambana mengine yakitokea nchi jirani.

Hata taarifa ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kwamba kituo kikuu ambapo dhahabu ya Afrika huteremshwa ni Umoja wa Falme za kiarabu UAE, lakini mnamo mwaka 2015 China iliingiza nchini mwaka kiwango kikubwa cha dhahabu kutoka Afrika kuliko nchi hiyo ya kiarabu.

Hata hivyo, mnamo mwaka 2016 nchi hiyo ya UAE iliingiza dhahabu kutokaa Afrika yenye thamani ya dola bilioni 15.1, ambapo mshauri mwandamizi wa maendeleo ya viwanda wa Umoja wa Afrika, Frank Mugyenyia alisema kiwango kikubwa cha dhahabu kinauzwa nje ya Afrika bila ya daftari.

Katika muongo mmoja uliopita kumekuwa na mahitaji makubwa ya dhahabu, hali ambayo imesababisha utoroshwaji wa dhahabu barani Afrika na kupelewa barani Ulaya, Marekani na nchi za Asia.

Kuongezeka kwa mahitaji ya dhahabu kumesababsia Afrika kutoambulia faida za mali hiyo, huku pia nchi za Kiafrika zikikabiliwa na jeraha la uwepo wa uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo ya migodi.

Vifaa vinavyotumiwa na wachimbaji wa dhahabu vinaongeza uzalishaji, lakini katika mchakato wa kuchimba dhahabu hiyo maji ya sumu yanaingia kwenye mito na kuathiri afya za watu wanaotumia maji hayo.

Maji hayo ya sumu yanasababisha maradhi kwenye ini, mafigo, bandama na mapafu, ambapo serikali za Afrika zinajaribu kutafuta njia ya kuisimamia sekta hiyo kwa sababu inawaingizia wananchi wengi mapato.

Kwa mfano nchini Tanzania taarifa ya bunge imeonyesha kwamba asilimia 90 ya dhahabu inayozalishwa nje ya taratibu rasmi, inatoroshwa nje ya nchi ya nchi hiyo.

Serikali ya nchi hiyo imeitaka benki kuu inunue dhahabu kutoka kwa wachimbaji, ambapo pia inapanga kuanzisha vituo rasmi vya biashara ya dhahabu.

Bei ya dhahabu sasa inafikia dola 40,000 kwa kilo. Kadri inavyotoroshwa na kuuzwa nje, nchi za Afrika zinaingia hasara ya mabilioni kila mwaka, kwa mujibu wa uchunguzi wa shirika la Reuters.