NA MARYAM HASSAN

KIJANA Mohammed Idrissa Mussa (53) mkaazi wa Mshelishelini, ameshindwa kuwasilisha wadhamini wawili kwa ajili ya kumdhamini juu ya kesi yake ya kukashifu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane.

Masharti hayo yametolewa na Hakimu wa mahakama ya mkoa Vuga Hamisuu Saaduni Makanjira, ambapo alimtaka mshitakiwa huyo kuwasilisha wadhamini hao ambao watasaini bondi ya shilingi 2,000,000.

Pia Hakimu huyo alisema, wadhamini hao wawasilishe kopi ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi pamoja na barua ya Sheha wa Shehiya wanazoishi.

Huku mshitakiwa mwenyewe alitakiwa kusaini shilingi 100,000 taslimu na akishindwa aende rumande hadi Agosti 3 mwaka huu kesi yake itakapoanza kusikilizwa ushahidi.

Hatua ya kupewa masharti hayo, imekuja kufuatia mshitakiwa huyo baada ya kusomewa hati ya mashitaka na kuomba kupewa dhamana.

Hati hiyo imesomwa na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Mohammed Abdalla, ambae hakuwa na shaka juu ya kupewa dhamana mshitakiwa huyo.

Wakili huyo alisema, mshitakiwa ana haki ya kupewa dhamana, lakini katika masharti atayopewa yawe madhubuti na yenye kutekelezeka.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka inaeleza kuwa, mnamo mwezi wa 11 mwaka jana majira ya saa 3:00 za usiku huko Beit el ras wilaya ya Magharibi ‘A’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa bila ya halali alimkashifu mtoto huyo kwa kumvua nguo zake za ndani, kisha kumtia vidole katika sehemu zake za siri za mbele jambo ambalo ni kosa kisheria.

Hivyo mshitakiwa amepelekwa rumande hadi Agosti 3 mwaka huu kwa ajili ya kesi yake kuanza kusikilizwa ushahidi.