NA MARYAM HASSAN

KIJANA aliyedaiwa kumtorosha mshichana wa miaka 16, kwa kumtoa nyumbani kwao Kizimbani na kumpeleka kwenye Mikungumanga huko huko Kizimbani, ametakiwa kujidhamini kwa bondi ya shilingi 500,000.

Amri hiyo imetolewa na Hakimu wa mahakama ya mkoa Vuga Salum Hassan, baada ya mshitakiwa huyo kuomba kupewa dhamana kutokana na kosa aliloshitakiwa nalo.

Hakimu huyo alimtaka mshitakiwa kujidhamini kima hicho cha fedha pamoja na kuwa na wadhamini wawili, ambao kila mmoja atasaini kima hicho hicho pamoja na kuwasilisha kopi za Kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi pamoja na barua ya Sheha wa Shehiya anayoishi.

Kabla ya kutolewa kwa masharti hayo ya dhamana, upande wa mashitaka chini ya wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Shamsi Saad Yasiin, ulisema kosa aliloshitakiwa nalo mshitakiwa huyo linadhaminika hivyo kwa upande wao hauna shaka na dhamana.

Aliiomba mahakama kutoa masharti madhubuti dhidi yake, ambayo yataweza kumfikisha mahakamani kila atakapohitajika.

Baada ya kutoa maelezo hayo, aliiomba mahakama kuiahirisha kesi hiyo na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa, kwa sababu upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika.

Mshitakiwa wa shauri hilo ni Kassim Charles Madafu (18) mkaazo wa Kizimbani, ambaye alishitakiwa mahakamani hapo kwa kosa la kutorosha msichana wa miaka 16.

Tukio hilo anadaiwa kulitenda Disemba mwaka jana majira ya saa 7:00 za mchana, huko Kizimbani ambapo alidaiwa kumtorosha msichana huyo ambaye hajaolewa na yupo chini ya uangalizi wa wazazi wake, jambo ambalo ni kosa kisheria.