NA MARYAM HASSAN

BAADA ya kufikishwa mahakamani kwa kosa la kumfanyia shambulio la aibu mtoto wa kiume wa miaka sita, hatimae Said Sleyum Abdalla umaarufu ‘Anco kocha’ (52) mkaazi wa Welezo, amerudia uraiani.

‘Anco kocha’ amerudi uraiani baada ya kukamilisha masharti ya dhamana aliyopewa na mahakama ya mkoa Vuga, dhidi ya shitaka hilo aliloshitakiwa nalo mahakamani hapo.

Masharti hayo ni yeye mwenyewe kusaini bondi ya shilingi 1,000,000 pamoja na kudhaminiwa na wadhamini wawili waliosaini kima hicho hicho cha fedha kila mmoja, huku wakiwasilisha barua za Sheha wa Shehiya wanayoishi na vivuli (kopi) vya vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Kabla ya kutolewa masharti hayo, mshitakiwa huyo aliiomba mahakama impatie dhamana ombi ambalo halikuwa na pingamizi mahakamani hapo.

Ombi hilo aliliwasilisha mara baada ya upande wa mashitaka kuomba kesi hiyo iahirishwe na kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa, kutokana na upelelezi wake tayari umeshakamilika.

Upande wa mashitaka, chini ya Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ahmed Mohammed, haukua na shaka na ombi hilo la mshitakiwa.

Ulisema hauna pingamizi juu ya kupewa dhamana mshitakiwa huyo, lakini aliiomba mahakama kutoa masharti madhubuti dhidi yake, ili siku ikitokea ameshindwa kuhudhuria mahakamani awepo mtu wa kutoa taarifa zake.

Mapema akiwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Valentine Andrew Katema, mshitakiwa huyo alishitakiwa kwa kosa la shambulio la aibu.

Kosa hilo anadaiwa kulitenda Januari 22 mwaka huu majira ya saa 3:00 za usiku, huko Welezo wilaya ya Magharibi ‘A’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Siku hiyo bila ya halali, alidaiwa kumsugulia sehemu zake za siri za mbele katika sehemu za siri za nyuma za mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka sita (jina linahifadhiwa), jambo ambalo ni kosa kisheria.

Baada ya kusomewa maelezo hayo alikataa, upande wa mashitaka ulidai upo tayari kuthibitisha tuhuma hizo dhidi yake na kuomba kesi iahirishwe na kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 3 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa na mahakama imeuagiza upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.