NA MARYAM HASSAN

JESHI la Polisi mkoa wa Kusini Unguja, limempandisha mahakamani kijana Hemed Salum Hemedi (45) mkaazi wa Bambi, kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya.

Kijana huyo alipandishwa mahakamani hapo kufuatia kufanyika kwa operesheni maalum ya kupambana na watumiaji, wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya katika mkoa huo.

Hemedi alisomewa shitaka lake na Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ayoub Nassor, kwamba alipatikana na dawa hizo Juni 13 mwaka jana.

Wakati operesheni hiyo inafanyika, Jesi la Polisi majira ya saa 5:30 za usiku lilimshikilia kijana huyo huko Bambi bondeni wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Shauri hilo lilisomwa mbele ya Hakimu Saidi Hemed Khalfani wa mahakama ya mkoa Mwera.

 Mshitakiwa alipatikana na dawa za kulevya aina ya Heroin kete 52 alizokuwa amezihifadhi kwenye karatasi ya mng’aro ‘alminium Foil’ na kuzitia kwenye kifuko cheupe zikiwa na uzito wa gramu 0.918 jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aliposomewa shitaka lake mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana, jambo ambalo lilikubaliwa mahakamani hapo.

Hakimu Said, alimtaka mshitakaiwa huyo kusaini bondi ya shilingi 2,000,000 pamoja na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao watasaini kima hicho hicho pamoja na kuwasilisha barua ya Sheha na kopi ya kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi.

Baada ya kupewa masharti hayo mshitakiwa alishindwa kuyatekeleza na badala yake kesi hiyo imeahirishwa hadi Ogasti 5 mwaka huu na mshitakiwa amepelekwa rumande.