MADRID, Hispania.
WAKALA wa winga wa kimataifa wa Wales, Gareth Bale, amesema, mteja wake wala hana mpango wa kuachana na Real Madrid, lakini tatizo liliopo ni kwamba kocha, Zinedine Zidane, hataki kumchezesha.

Wakala, Jonathan Barnett, amesisitiza kwamba Bale haondoki kwenye kikosi hicho, licha ya msimu huu kusugua benchi muda mrefu huku timu hiyo ikibeba ubingwa wa ‘La Liga’.
Nyota huyo hakucheza mechi yoyote kwenye klabu hiyo katika michezo yao saba ya mwisho, ambapo walifanikiwa kubeba taji lao la 34 la Ligi Kuu ya Hispania.

Winga wa zamani wa Tottenham Hotspurs na Manchester United, Dimitar Berbatov, alimshambulia Bale kwa kumwambia amejifanya si kama mwanasoka wa kulipwa baada ya kuigiza kulala akiwa benchi huku timu yake ikicheza huku picha nyengine zikimuonyesha akiwa ameigiza kushika darubini.

Lakini, wakala Barnett, alisema kwa msisitizo ‘haendi popote”.
Barnett alisema, Bale, anayelipwa pauni 600,000 kwa wiki, hataondoka kwa mkopo au kwa uhamisho wa jumla kama hakutakuwa na ofa nzuri kutoka kwenye klabu nyengine.
“Gareth yupo sawa tu. Ana miaka miwili kwenye mkataba wake. Anapenda kuishi Madrid, hivyo, haendi popote”, alisema, Barnett.
“Bado yupo vizuri kama ilivyo wachezaji wengine kwenye timu. Ni mambo ya Zidane tu. Sawa, kuna timu zinamtaka, lakini ni ngumu kupata timu hapa duniani itakayoweza gharama zake.
“Ni huzuni kubwa kwamba hapati nafasi kwenye kikosi cha sasa cha Real Madrid, lakini hataondoka.”

Barnett, alisema, hakuna ugomvi wowote baina ya Zidane na Bale, lakini, kocha huyo wa Kifaransa hataki
kumchezesha.
Zidane aliwahi kusema kwamba hana tatizo na Bale na kwamba alimuondoa kwenye timu katika mechi ya
mwisho kutokana na mambo ya kiufundi tu.(Goal).