OTHMAN KHAMIS

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema wananchi wanapaswa kuzitumia fursa zinazopatikana kupitia Utamaduni wao, kama nyenzo muhimu ya Biashara, Ajira na Uchumi wakiendelea kulinda Mila na Ahlaki njema zinazotokana na utamaduni huo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kulinda na kuendeleza misingi na maelekezo ya kiutekelezaji, yanayotokana na miongozo mbali mbali katika kuhakikisha utamaduni wa Taifa unaenziwa wakati wote.

Akilifungua Tamasha la 25 la Utamaduni wa Mzanzibari hapo Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Michenzani Square Balozi Seif Ali Iddi, alisema mchango wa tasnia ya sanaa na ubunifu katika uchumi wa Zanzibar inakisiwa kuwa asilimia 4.3%  kutoka Mwaka 2010 hadi 2018.

Balozi Seif alieleza kwamba hiyo ni hatua nzuri iliyofikiwa na tasnia hii katika kuchangia uchumi wa Taifa huku akizitaka Taasisi zinazohusika na Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa kuendelea kujenga mazingira bora zaidi kwa Wazalishaji wa Kazi na bidhaa za Sanaa ili waweze kuyafikia malengo na matarajio ya Taifa.

Alitoa wito kwa Jamii ikubaliane na mabadiliko hayo na kutambua kwamba sanaa na utamaduni ni kazi kama zilivyo kazi nyengine katika mfumo wa kibiashara ambazo zinalindwa kwa misingi ya utaratibu wa Kisheria.