NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
MJUMBE wa kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM, Balozi Seif Ali Iddi amesema kigezo cha uongozi bora wa kuutumikia umma kinapimwa kutegemea umahiri wa mtu aliyeshiba uzalendo unaothubutu kuwa tayari kusimamia maendeleo ya wale aliokubali kuwasimamia.
Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati akitoa salamu kwenye mkutano mkuu wa CCM jimbo la Mahonda wa kupiga kura za maoni kwa wagombea wa ubunge na uwakilishi kupitia chama hicho.
Mkutano huo uliosimamiwa na wawakilishi wa CCM wilaya ya Kaskazini ‘B’ umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja iliyopo Mahonda.
Balozi Seif akiwa mjumbe wa mkutano huo aliyemaliza muda wake wa ujumbe wa baraza la wawakilishi alisema wajumbe hao wana kazi nzito ya kumchagua mwanachama atakayeendeleza maendeleo yaliyopatikana.
Alisema kura za wajumbe hao ambazo zina thamani ya kipekee hasa ikizingatiwa kuwa zina uwezo mkubwa wa kubainisha ni kwa kiasi gani yule waliyemteua ameshiba umahiri wa kuwasimamia vyenginevyo ni kudumaa kwa maendeleo ya jimbo hilo.
“Nitafurahi sana iwapo tutawachagua wanachama wenzetu walio mahiri na nguvu za kizalendo zitakazoyaendeleza yale mazuri tuliyoyakuta na kuyaacha sisi kwa mustabali wa umma”, alisema.
Mjumbe huyo wa kamati kuu ya halmashauri kuu ya Taifa ya CCM aliwapongeza wananchi na wana CCM wa jimbo la Mahonda kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chake chote cha miaka mitano.
Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi jimbo la Mahonda, Farahan Haji Othman akiufungua mkutano huo alisema uchaguzi ni matokeo yanayopembua wanaogombea au kushindania nafasi.
Farahan alisema mchakato huo hubeba makundi mbali mbali ya waomba nafasi hizo ni vyema pale unapofikia wakati wa kumpata mmoja miongoni mwao kinachoendelea mbele ni makundi yote kurejea katika umoja na mshikamano.
Mchakato huo wa kura za Maoni ndani ya jimbo la Mahonda umewashirikisha waomba ridhaa wapatao 15 kwa nafasi ya kugombea ujumbe wa baraza la Wawakilishi na 15 kwa nafasi ya bunge kupitia CCM.