NA MWANAJUMA MMANGA

VIONGOZI wa Baraza la Vijana Magharib ‘A’ wametakiwa kuzingatia taaluma inayotolewa ya ufugaji nyuki kupitia mradi wa uzalishaji asali, kwani utaweza kuwajengea vijana wao  kujiajiri wenyewe  na kuondokana na kusbiri ajira serikalini.

Ushauri huo, umetolewa na Katibu wa Baraza la Vijana Wilaya hiyo, Amina Mohamed Waziri, wakati walipofanya ziara ya kujifunza kazi za ujasiriamali ikiwemo ya uzalishaji asali eneo la Fuoni Kibondeni.

Alisema iwapo watafuga nyuki hao kwa wingi wataweza kuzalisha asali na kujikwamua na hali ngumu za umaskini hapa nchini.

“Lengo la ziara hiyo ni kuona mradi huu ni kujifunza kazi ya ujasiriamali ya  ufugaji wa nyuki, kuongeza  uzalishaji wa asali lakini pia unaleta manufaa kwao” alisema

Alisema kazi ya ufugaji nyuki inahitaji mbinu ambayo itaweza kuwaletea tija kwao, kwani ina manufaa makubwa katika kuinua kipato iwe cha mtu mmoja mmoja ama kwa serikali.

Alisema serikali imekuwa ikitoa mafunzo mbali mbali juu ya namna ya ufugaji nyuki, hivyo ni vyema kushajiika kikamilifu ufugaji nyuki kuongeza tija. 

Alisema kuwa wafugaji wengi wamekuwa wakikata tamaa ya ufugaji nyuki kutokana na wakati wanapotega mizinga yao kuingia ndege wengine badala ya nyuki wanaotegwa.