NA MWANAJUMA MMANGA
KATIKA miaka ya hivi karibuni kumejitokeza tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuweka mbele maslahi yao kuliko afya na maisha ya watu kutokana na kuuza bidhaa feki au zilizo maliza muda wa matumizi.

Bidhaa hizo zimezagaa maeneo kadhaa ya mijini na mashamba na kwamba ziko sokoni kama kawaida jambo ambalo wananchi wanazinunua bila ya kujua athari zake.

Wako baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakifoji kwa makusudi kwa kubadilisha muonekano wa awali na kuufanya mpya ma kuingiza katika kifaa chengine kinaonekana ni kipya kabisa.

Kwa mfano vitu vya nafaka kama mchele hubadilishwa kwenye mapolo mapya na baadae kuandikwa tarehe mpya ya kumaliza muda wake wa matumizi.

Halkadhalika kwa bidhaa za makopo, vimimika kama mafuta hufanywa mtindo kama huo na hivyo kupelekea afya za watumiaji kuwa rehani.

 nna kujifanya wajanja wa kuingiza vyakula viliokosa ubora hapa Zanzibar.
Baadhi ya vyakula hivi viliopita muda wake wa matumizi au kukosa ubora unaotakiwa vimekuwa vikiathiri maisha ya watu wa Visiwani.

Pamoja na jitihada kubwa za Serikali kupambana na bidhaa feki au zilizopitwa na wakati bado kunaonekana kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaokiuka sheria na kuendeleza biashara hiyo.

Uamuzi wa baadhi ya wafanyabishara kupingana na maagizo ya serikali yanayotolewa mara kwa mara juu ya umuhimu wa kuingiza bidhaa na vifaa vyenye ubora kwa matumizi wa wananchi umepelekea kuibuka kwa maradhi mbali mbali.

Miongoni mwao ni ya ngozi, matumbo na saratani.

Utafiti unaonyesha mara nyingi maradhi ya saratani huchochewa na ulaji wa vyakula  vibovu au kutumia vifaa bandia na vyenye ubora hafifu.

Baadhi ya vifaa vibovu vinachangia pakubwa uchafuzi wa mazingira ambao tunauona katika maeneo mbali mbali ya visiwa vyetu.
Kwa mfano, hivi karibuni gazeti hili liliripoti kuwepo kwa bidhaa bandia ya dawa ya kutakasa mikono (sanitizer) na vikinga mdomo (mask) ambazo hazina ubora.

Lengo la bidhaa za maski na vitakasa mikono ni kujikinga na gonjwa hatari la mafua makali yanayosababisha homa ya mapafu yaani corona lakini kwa kushangaza baadhi ya wafanyabiashara wajanja wametumia fursa hii kuwarubuni watu kwa maslahi yao.

Vifaa hivi ambavyo ni sehemu ya vitu muhimu vinavyotumika katika vita dhidi ya maradhi ya Covid 19, havikupaswa kuwa hata kidogo chini ya ubora kwani inaweza kuwa chanzo cha kukuza maradhi badala ya kusaidia kukinga ugonjwa huo ulioingia nchini toka mwezi machi mwaka huu.