ABUJA, NIGERIA

MAOFISA wa usalama nchini Nigeria wametangaza kuwa, idadi ya wanajeshi wa nchi hiyo waliouawa kufuatia shambulio la kundi la kigaidi la Boko Haram katika mji wa Maiduguri wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo imeongezeka na kufikia 35.

Taarifa ya jeshi la Nigeria imeeleza pia kuwa, mbali na idadi hiyo ya wanajeshi kuuawa kuna wanajeshi wengine 30 ambao bado hawajulikani walipo baada ya shambulio la kushtukiza la Boko Haram Jumanne iliyopita.

Awali jeshi la Nigeria lilikuwa limetangaza kuwa, wanajeshi wake 23 wameuawa katika shambulio dhidi ya wanajeshi hao, na baadaye kubainika kuwa wengine walikuwa wametoweka.

Afisa mmoja wa kijeshi amewaambia waandishi wa habari kwamba, wanajeshi 35 wameuwa, 18 wamejeruhiwa na wengine 30 hawajulikani walipo.

Wakati huo huo kwa mujibu wa jeshi la Nigeria wanachama 17 wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameuawa pia katika mapigano yaliyozuka baada ya shambulio la magaidi hao.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni jeshi la Nigeria lilitangaza habari ya kuuawa wanachama 75 wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika operesheni 17 zilizofanyika baina ya Juni Mosi na Juni 30 mwaka huu.

Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa ambapo, eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria limekuwa uwanja wa mashambulizi ya wanachama wa kundi la kigaidi Boko Haram ambao mwaka 2014 waliteka nyara mamia ya wasichana katika shule moja ya sekondari mjini Chibok.

Zaidi ya watu 30,000 wameuawa na wengine wanaokaribia milioni tatu wamelazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kundi hilo la Boko Haram nchini Nigeria tokea mwaka 2009.