NA ALI SHAABAN JUMA

BENJAMIN William Mkapa aliyekuwa Rais wa Tanzania kwa miaka 10 kuanzia   Novemba 23 mwaka 1995 hadi mwaka 2005 amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 siku ya Ijumaa ya tarehe 24 Julai, 2020. Katika Makala haya, mwandishi Ali Shaaban Juma anaelezea kwa ufupi historia ya mwanasiasa huyo.

Benjamin William Mkapa alizaliwa tarehe 12 Novemba 1938, Masasi, Mtwara na kupata elimu ya msingi ya darasa la kwanza hadi la nne katika shule ya msingi la Lupaso kati ya mwaka 1945-1948.

Baadae alisoma darasa la tano hadi la sita katika skuli ya msingi ya Ndanda kati ya mwaka 1949-1951. Baada ya kumaliza masomo katika skuli ya msingi ya Ndanda, Mkapa aliendelea na masomo yake ya darasa la saba hadi la nane katika skuli ya seminari ya Kigonsera kati ya mwaka 1952-1953.

Baadae, hapo mwaka 1954, alisoma katika shule ya Sekondari ya Ndanda na kupata cheti cha kumalizia darasa la kumi. Kati ya mwaka 1955-1962, Benjamin Mkapa alisoma katika skuli ya sekondari ya Mtakatifu Francis ya Pugu mjini Dar es Salaam na kutunukiwa cheti cha Sekondari cha Cambridge.

Mkapa alikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi  waliosomeshwa  na  Mwalimu Julius Nyerere katika skuli ya Mtakatifu Francis  ya Pugu mjini Dar es Salaam.

Katika mwaka 1962, Mkapa alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda na kusoma hatua ya Preliminary Arts na kisha shahada ya kwanza ya Bachelor of Arts na kuhitimu hapo mwaka 1962 katika mchepuo wa kiingereza.

Wasiasa wengine mashuhuri wa Afrika Mashariki waliosoma Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda enzi hizo ni pamoja na Mwalimu Julius Nyerere, Aboud Jumbe Mwinyi, Idrisa Abdul Wakil, aliyekuwa Rais wa Kenya, Mwai Kibaki na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Uganda, Sipecioza Kazibwe.

Mkapa alianza kazi ya ofisa Tawala na ofisa wilaya katika wilaya ya Dodoma kati ya Aprili hadi Agosti, 1962.  Baadae kati ya mwezi wa Agosti, 1962- Mei,1963 alikuwa ofisa, mambo ya nje katika wizara ya nje mjini Dar es Salaam. 

Ni katika kipindi hicho ambapo Benjamin Mkapa na alihudhuria mafunzo maalum kwa ajili ya wanaplomasia kutoka nchi changa yaliyoandaliwa na kitivo cha masuala ya kimataifa ya Chuo Kikuu cha Colombia mjini New York huko Marekani.  Alijunga na Jeshi la Kujenga Taifa katika kambi ya Ruvu hapo mwaka 1971.

Mkapa, alikuwa Mhariri Mtendaji wa magazeti ya serikali ya “The Nationalist” na Uhuru, kati ya Mei 1966- Aprili,1972. Mbali ya kuwa Mhariri Mtendaji wa magazeti hayo, pia Mkapa alikuwa Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Daily News na Sunday News kwa miaka miwili kuanzia 1972-1974.

Rais wa Zanzibar, Bwana Aboud Jumbe (mwanzo kulia) akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akizungumza na wandishi wa habari kutoka Tanzania Bara walipotembelea Zanzibar hapo mwaka 1974. Mwanzo kushoto (aliyevaa miwani) ni Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Daily News na Sunday News Ndugu Benjamin Mkapa.

Baadae kwa miaka miwili kati ya mwaka 1974-1976, alikuwa mwandishi wa habari wa Rais Julius Nyerere katika Ikulu ya mjini Dar es Salaam. Benjamin Mkapa ni Mkurugenzi mwanzilishi wa Shirika la Habari la Tanzania (SHIHATA), ambapo alikuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo kati ya Julai- Oktoba 1976. Kabla ya hapo, tayari Mkapa alikuwa mbunge wa bunge la Afrika Mashariki kati ya mwaka 1969-1977.

Alijiunga na Chama cha Mapinduzi tarehe 1 Aprili, 1977 ambapo kadi yake   ya uanachama ilikuwa ni nambari B. 132201. Mkapa, alikuwa balozi wa Tanzania huko Nigeria, kati ya Oktoba 1976- Februari 1977.

Kati ya Februari, 1977-Okotoba, 1980 Mkapa alikuwa mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Nje wa Tanzania. Benjamin Mkapa alichukua nafasi ya Waziri wa Nje ambayo kabla yake ilishikiliwa na Ibrahim Kaduma (marehemu).

Mheshimiwa Mkapa ambaye alikuwa ni Waziri wa Nje wa saba wa Tanzania tokea muungano wa Tanganyika na Zanzibar hapo mwaka 1964, alihamishwa katika wizara hiyo hapo mwaka 1980 na nafasi hiyo ilishikiwa na Dk. Salim Ahmed Salim aliyeshikilia nafasi hiyo kwa miaka mitatu hadi mwaka 1984.

Mbali ya kuendelea kuwa mbunge wa kuteuliwa pia alikuwa na waziri wa Habari na Utamaduni wa Tanzania kati ya Novemba 1980-Februari, 1982.

Benjami Mkapa alikuwa balozi wa Tanzania nchini Canada kati ya Aprili 1982-Februari,1983 na baadae alihamishiwa nchini Marekani ambako alikuwa balozi kati ya Februari 1983- Aprili,1984. Akiwa bado katika Wizara ya Nje, Mkapa alikuwa mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Nje, kati ya Aprili 1984- Oktoba, 1985.

Ni katika kipindi hicho ndipo alipochaguliwa kuwa mbunge wa kuchaguliwa wa jimbo la Nanyumbu na waziri wa Nje kati ya Oktoba 1985-Oktoba 1990. Aliendelea kuwa Mbunge wa jimbo la Nanyumbu kwa miaka mitano mengine kati ya Oktoba 1990-Oktoba 1995.

Kati ya Novemba 1990 hadi Mei,1992 alibadilishwa wizara na kuwa waziri wa Habari na Utangazaji, kati ya Novemba 1990- Mei,1992. Kisha aiteuliwa kuwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu kati ya Mei 1992 hadi Novemba,1995. Mkapa, alikuwa mjumbe wa kamati kuu ya CCM kati ya mwaka 1977-1982.

Mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi kumchagua mgombea urais wa Tanzania kwa chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 1995, ulifanyika mjini Dodoma hapo tarehe 24 Julai, 1995 ambapo waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo na kuzirejesha walikuwa ni wanachama 17.

RAIS Nyerere akimuapisha Ndugu Benjamin Mkapa kuwa balozi wa Tanzania huko Nigeria Ikulu mjini Dar es Salaam hapo mwaka 1976. Katikati ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu, Bwana Timony Apiyo.

Wanachama wawili walikatwa majina yao katika hatua za awali na kubaki wagombea 15. Baadhi ya wagombea waliojitokeza kugombea nafasi hiyo   walikuwa ni pamoja na John Malecela, Edward Lowassa, Cleopa Msuya na Jakaya Kikwete.

Baada ya mchujo kufanywa na chama hicho, kati ya wagombea hao 15 yalibaki majina matatu ambayo yalikuwa ni Jakaya Mrisho Kikwete, Cleopa Edward Msuya na Benjamin William Mkapa ambaye kwa wakati huo, alikuwa ni Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu.

Kura zilizopigwa na mkutano mkuu huo wa CCM wa Julai, 1995, zilimpitisha Benjamin Mkapa kuwa mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi.

Uchaguzi huo wa Rais wa Tanzania ulifanyika siku ya Jumapili tarehe 29 Oktoba, 1995 ambapo wagombea Urais wa Tanzania walikuwa ni Benjamin Mkapa wa CCM, Augostino Mrema wa NCCR Mageuzi, John Cheyo wa UDP na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF.

Benjamin Mkapa alitangazwa kuwa Rais wa Tanzania hapo tarehe 22 Novemba,1995 baada ya kuwashinda wapinzani wake kwa kupata kura 6,846,681 ambazo ni sawa na asilimia 61.8% ya kura zote.

Katika uchaguzi huo, Augstino Mrema wa chama cha NCCR – Mageuzi alipata kura 1,808.616 sawa na asilimia 6.4% na John Cheyo wa UDP alipata kura 258,734 sawa asilimi 4.0%.

Kutokana na katiba ya Tanzania kifungu cha 42, kifungu kidogo cha 3 (a) rais anaruhusiwa kubaki madaraknai hadi siku ambayo Rais mteule atakula kiapo.

Hivyo basi Rais Ali Hassan Mwinyi ambae alishikilia wadhifa huo kwa miaka kumi kuazia mwaka 1985 hadi 1995 hakuruhusika tena kugombea cheo hicho kwa mujibu wa katiba ya Tanzania. 

RAIS wa Tanzania, Mwalimu Nyerere(katikati) akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Salim Ahmed Salim (kulia) katika mkutano wa kimataifa hapo mwaka 1984. Kushoto ni Waziri wa Nje wa Tanzania, Ndugu Benjamin Mkapa.

Rais Ali Hassan Mwinyi alimaliza muda wake wa uongozi hapo tarehe 23 Novemba, 1995 siku ambayo Rais Benjamin Mkapa alipoapishwa rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi kupitia akiongoza Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi.

Mkapa alikuwa Rais wa Tanzania kwa miaka kumi kuanzia tarehe 23 Novemba, 1995 hadi siku ya Jumatano ya tarehe 21 Disemba, 2005 alipoapishwa Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Rais wa Tanzania.

Miongoni mwa miradi mikubwa iliyotekelezwa nchini Tanzania na Rais Mkapa alipokuwa madarakani ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa kisasa uliojengwa mjini Dar es Salaam.

Wakati wa maadhimisho ya sherehe za miaka 40 ya uhuru wa Tanzania Bara, Rais Mkapa aliahidi kujenga uwanja wa michezo wa kisasa kwa ajili ya michezo mbalimbali. Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 ndio sura ya michezo nchini Tanzania hivi sasa.

Taasisi ya Benjamin Mkapa inayotoa huduma za afya katika maeneo mbalimbali Tanzania, iliyoazishwa hapo mwaka 2005 ni moja kati ya kumbukumbu za kitaifa za kiongozi huyo.

Benjamin William Foundation was established after the launching of its first initiative known as the 2005.