SAFARI ya miaka 81 hapa duniani ya rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa imehitimika rasmi jana baada ya kuzikwa kijiji kwake Lupaso, wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.

Tangu afariki dunia mnamo Julai 24 mwaka huu, watu wengi waliopata nafasi kwenye vyombo vya habari na sehemu nyengine mbalimbali, wameyaelezea maisha ya mzee Mkapa.

Mambo mbalimbali mazuri yaliyoelezwa kuhusu mzee Mkapa yakiwemo jinsi alivyo watetetea kuwapigania, kujenga uzalendo nakadhalika, inaonesha ndio uhalisia wa wema wake.

Sisi kama chombo cha habari tunamkumbuka Mkapa kutokana staili yake ya uongozi, kwani alihakikisha anawahimiza watanzania kufanya kazi, wanajituma, alichukia rushwa, alipambana na wakwepa kodi pamoja na dhuluma nyengine.

Wakati wa uongozi wake mzee Mkapa aliwaunganisha watanzania na kuendelea kuwonya dhidi ya ubaguzi miongoni mwao ukiwemo wa ukabila na wa kidini.

Mzee Mkapa huyu huyo, ndiye aliyenga misingi imara ya kiuchumi ambapo mwezi mmoja kabla ya kifo chake Tanzania ilitangazwa na benki ya dunia kuwa imeingia kwenye uchumi wa kipato cha kati.

Tunamkumbuka vyema mzee Mkapa jinsi alivyokuwa muumini mzuri wa muungano wa Tanzania, ambaye kiukweli alisimamia vyema jukumu lake katika eneo hilo.

Mzee Mkapa pia alikuwa akiamini dhana nzima ya kujikomboa na kuchukia madhila na manyanyaso ya ukoloni, ndio maana hatukumshangaa kumuona akiyakubali, kuyaunga mkono, kuyapigania na kuyatetea mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Kwa hakika mzee Mkapa ni kiongozi aliyejaliwa kuwa na vipaji vingi ikiwemo diplomasia ambayo ni moja ya taaluma aliyoitendea haki, ndio manaa alishiriki kikamilifu kwenye usimamizi wa miafaka ya kisiasa Zanzibar.

Fani hiyo ya diplomasia aliifanyiakazi hadi nje ya Tanzania kwani alishiriki kikamilifu kuupatia suluhu mgogoro wa kisiasa nchini Kenya wa mwaka 2007 uliotokana na uchaguzi mkuu.