PARIS, Ufaransa
BAADA ya Mahakama ya Usuluhishi Michezoni (CAS) kutengua maamuzi ya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) kuifungia Manchester City kushiriki michuano ya bara hilo kwa miaka miwili, meneja Pep Guardiola, ameibuka na kutoa kauli nzito.

Uongozi wa ManCity ulikata rufaa CAS kupinga uamuzi wa Uefa, kwa kuamini hawakutendewa haki wakati wa kutangazwa hukumu mapema mwaka huu, kufuatia tuhuma za matumizi mabaya ya fedha na udanganyifu mkubwa katika makusanyo ya mapato ya klabu (FFP), pamoja na kutotoa ushirikiano kwa timu iliyokuwa inafanya uchunguzi wa matumizi mabaya ya fedha mwaka 2012-2016.

Guardiola ameibuka na kusema Uefa inatakiwa kuiomba radhi klabu hiyo ya mjini Manchester, England kufuatia uamuzi dhahir ulionekana haukuwa wa haki.

“Kilichofanyika ni haki, lakini, makocha wote hapa ni lazima wajue kuwa tunahitaji haki na bila ya shaka haki imetendeka. Nadhani kuna haja ya kuombwa radhi kwa makosa yao”, alisema, Guardiola.
Uefa ilitoa hukumu juu ya ManCity ya kutoshiriki michuano ya Ulaya hata kama wangelifuzu na matajiri hao wa jiji la Manchester sasa watakuwa sehemu ya washindani kwenye michuano ya Uefa.(Goal).