NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
HATUA za kuimarisha uchumi zilizochukuliwa na serikali zimeleta mafanikio katika kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo uliochangiwa zaidi na uwepo wa hali ya amani na utulivu nchini.
Akiwasilisha taarifa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM katika mkutano mkuu wa chama mjini Dodoma, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema hatua hiyo imeiwezesha serikali kutekeleza mipango ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani.
Alizipongeza taasisi zinazosimamia mapato; Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao na kufikia mafanikio ya kuridhisha .
Alisema katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2019, pato la taifa limekua kutoka thamani ya 1.768tr/- mwaka 2010 hadi kufikia thamani ya shilingi 3.078tr/- mwaka 2019.
Alieleza kwamba ongezeko hilo ni sawa na mara 1.74 zaidi ya wakati wa awamu ya saba inaingia madarakani ambapo kasi ya ukuaji uchumi imepanda kutoka asilimia 4.3 mwaka 2010 hadi asilimia 7.0 mwaka 2019.
Alisema pato la mtu mmoja mmoja nalo limeongezeka kutoka shilingi 942,000 sawa na dola za Marekani 675 mwaka 2010, hadi shilingi milioni 2.5 sawa na dola 1,114 mwaka 2019.
Aidha alisema, mfumko wa bei umeshuka kutoka asilimia 14.7 mwaka 2011 hadi asilimia 2.9 mwaka 2019 hali iliyoleta faraja kwa wananchi kupata bidhaa muhimu kwa bei ya kuridhisha wakati serikali kwa upande wake imefanikiwa kuongeza mapato mwaka hadi mwaka.
Alibainisha kwamba mapato ya ndani yalifikia shilingi bilioni 748.9 hadi mwaka 2019/2020, ikilinganishwa na shilingi bilioni 181.1 zilizokusanywa mwaka 2010/2011, hali iliyopunguza utegemezi wa bajeti kutoka wastani wa asilimia 30.2 mwaka 2010/2011 na kufikia wastani wa asilimia 5.7 mwaka 2018/2019.
Akizungumzia miundombinu, alisema jitihada zimechukuliwa kuimarisha ujenzi wa barabara ambapo tayari kilomita 129 zimekamilika katika kiwango cha lami.
Alisema hicho ni kiwango kikubwa kuwahi kujengwa katika historia ya Zanzibar kilichokwenda sambamba na ujenzi wa madaraja na kuweka taa barabarani na za kuongozea vyombo vya moto.
Alisema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na serikali kujikita zaidi katika ununuzi wa vifaa na zana za kisasa za kutengenezea barabara kazi iliyofanywa na wakala wa barabara Zanzibar.
Alieleza kwamba uimarishaji wa usafiri wa anga umezingatiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume na uwanja wa Karume Pemba kwa kujengwa njia za kupitia ndege kutoka mita 1,805 hadi mita za mraba 3,427.
Alisema wahandisi wa ujenzi kwa sasa wanakamilisha ujenzi wa jengo jipya la abiria la terminal 3 la uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume ambao una barabara ndefu ya kurukia ndege kuliko viwanja vyote vya Afrika Mashariki ambao utahudumia abiria 1.6 milioni kwa mwaka.
Akigusia nishati ya umeme alisema serikali katika awamu zake mbali mbali imefanya jitihada kadhaa za kuhakikisha Zanzibar inakuwa na huduma ya umeme wa uhakika.
Alisema katika jitihada zilizoanzishwa na awamu zilizotangulia za kusambaza na kuwafikishia wananchi huduma popote walipo, serikali imefikisha umeme katika shehia zote ambapo kwa sasa nishati hiyo inapatikana katika vijiji 2,882 kati ya 3,259, vikiwemo vijiji 354 vilivyopatiwa umeme katika kipindi hiki.
Alisema jumla ya visiwa vidogo vitano vimepatiwa huduma ya umeme ambavyo ni Kisiwapanza, Makoongwe, Shamiani, Fundo na Uvinje wakati jitihada za kuufikisha umeme katika visiwa vya Kokota na Njau zilikabiliwa na changamoto na kusababisha kuchelewa.
Hata hivyo, alisema fedha kwa ajili ya kazi hiyo zimetengwa na utekelezaji wa mpango huo utaendelezwa kama serikali ilivyoahidi na kuwanasihi wakaazi wa visiwa hivyo kuendelea kuwa na subira.
Alibainisha kwamba kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme, serikali imeamua kuwa ipo haja ya kuwa na umeme wa uhakika na tayari imeanza kutafuta njia mbadala za kupata vyanzo vipya vya nishati hiyo.
Alifahamisha kwamba utafiti uliofanywa na serikali chini ya wataalamu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) umeonyesha uwezekano mkubwa wa Zanzibar kupata nishati ya umeme wa jua.
“Benki ya Dunia itatuunga mkono kwa kuanzia kupata MW 35, lakini wapo wawekezaji waliojiandaa kuwekeza zaidi ya MW 70,” alisema.
Alisema hivi sasa serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo na tayari limefikia hatua nzuri kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na sekta binafsi, ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo.
Aliwapongeza viongozi pamoja na watendaji wote kwa kuendelea kuwajibika na kuwashukuru wananchi kwa ustahamilivu na imani yao kubwa kwa CCM na serikali zake zote mbili.