MADINA ISSA NA HAFSA GOLO
ZOEZI la kumpata mgombea wa nafasi ya ubunge wa jimbo la Mwanakwerekwe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) limekwenda vizuri baada ya juzi kusitishwa kutokana na kukosewa kwa karatasi za kura.
Zoezi hilo, lililofanyika jana kuanzia saa 3:30 asubuhi ambapo wajumbe na wagombea waliowania nafasi hiyo walielezea kuridhishwa kwao na matokeo hayo mara baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Msimamizi wa uchagzui huo Maabadi Ali Maulid, alisema uchaguzi huo umemalizika kwa kwa amani na utulivu ulikuwa mkubwa wakati wote.
Aliwashukuru wagombea walioingia katika mchakato huo na kusema kuwa hakuna mshindi na kwamba mchakato wa uteuzi wa wagombea unaendelea katika vikao vyengine vya chama.
Alisema kuwa mchakato huo ni hatua ya kwanza na wagombea wanaendelea kuchunguzwa na kumulikwa ambapo kitu chochote kinaweza kutokea katika mchakato huo.
Katika mchakato huo, aliyeongoza katika kura leo ni Kassim Hassan Haji ambae alipata kura 24.
Wakati huo huo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa jimbo la Donge wamepiga kura ya maoni kwa kuwachagua viongozi wa jimbo hilo kupitia nafasi ya Uwakilishi na Ubunge.
Zoezi hilo lilifanyika katika ofisi kuu ya Chama cha Mapinduzi Mkoa iliyopo Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja, Msimamizi wa uchaguzi huo, Kidawa Hamid Saleh alisema, wagombea wawili waliojitokeza kuwania uwakilishi na 22 waligombea ubunge jimboni humo.
Mapema kabla ya utekelezaji wa zoezi la upigaji kura msimamizi huyo aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanafata taratibu sambamba na kuheshimu maadili ya uchaguzi.
Msimamizi huyo alimtangaza Dk. Khalid Salum Mohamed kushika nafasi ya kwanza baada ya kupata kura 83 dhidi ya mshindani wake Khamis Amour Mussa aliepata kura 15.
Katika hatua nyengine Kidawa alimtangaza Soud Mohamed Juma kuwa alipata kura 33 na kuongoza katika mchakato huo kati ya kura 98 zilizopigwa.
Aliekuwa mbunge wa jimbo hilo Sadifa Juma Khamis kushika nafasi ya pili baada ya kupata kura 30 huku mgombea Fadhil Daud Ali alishika nafasi ya tatu baada ya kupata kura 19.