NA   ARAFA MOHAMED

MWENYEKITI wa Sekretarieti ya   Mkoa Abdallah Mwinyi   Hassan, amesema ni marufuku kwa watendaji wa ngazi wadi na Wilaya, kuwachangisha wagombeya wanaokwenda kuchukuwa fomu za  kuwania nafasi ya Udiwani, Uwakilishi na Ubunge kwa madai kuwa wanaimarisha chama.

Aliyasema hayo wakati alipokuwa akuzungumza na Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi wa Majimbo ya Magomeni, Jang’ombe, Kikwajuni na Malindi, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake yenye lengo la kutoa mafunzo kwa vikao vya uchujaji wa Majimbo tisa ya Mkoa wa Mjini kichama huko katika ukumbi wa tawi la (CCM)  Matarumbeta.

Alisema, utaratibu uliowekwa na chama wa uchukuwaji wa fomu kwa ngazi ya Udiwani ni shilingi 10,000,   nafasi ya Ubunge na Uwakilishi ni shilingi 100,000, hivyo si vyema kwa watendaji kuwachangisha wagombea hao, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na utaratibu uliowekwa na chama hicho.

Aidha alisema kuna baadhi ya watendaji walikuwa wakichangisha pesa kwa madai ya kutaka kukiimarisha chama, jambo ambalo halipo ndani ya chama cha Mapinduzi (CCM).

Abdallah ambae pia ni Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini, aliwataka viongozi wanaoshiriki katika vikao vya uchujaji kujifunza namna ya kuhifadhi siri za vikao, ili kuepuka migogoro inayoweza kujitoleza.