KWA muda sasa dunia imekuwa ikishuhudia kuongezeka kwa mvutano baina ya mataifa makubwa mawili duniani yenye nguvu za kiuchumi na kijeshi nayo ni Marekani na China.

Ingawaje mvutano huo upo kwa muda mrefu na sababu zake zinajulikana ikiwemo suala la utawala wa ulimwengu, lakini tangu rais Donald Trump aingie madarakani miaka minne iliyopita mvutano baina ya nchi hizo umezidi maradufu.

Katika mambo mengi ambayo tumeshuhudia yaliyosababisha kuzorota kwa kiasi kikubwa uhusiano baina ya Marekani na China, ni pamoja na kile kilichoitwa vita vya biashara.

Vita hivyo vinahusu suala la kupandishiana ushuru wa biadhaa zinazotoka baina ya taifa moja kuingia taifa jengine, hali ambayo pia ilitolewa maonyo na mashirika na jumuiya za kimataifa kuwa vita hivyo vinaweza kusababisha kuyumba kwa uchumi wa dunia.

Katika kile kinachoelezwa kuongezeka kwa mvutano baina ya China na Marekani, mnamo Julai 22 mwaka huu, utawala wa rais wa Marekani, Trump uliamuru kufungwa kwa ubalozi wa China uliopo katika jimbo la Houston kwneye mji wa Texas.

Kwa mujibu wa taarifa utawala wa Trump aliagiza kufungwa mara moja ubalozi huo ndani ya saa zisizozidi 48, ambapo China katika hatua za awali iliielezea hali hiyo kama uchokozi wa kisiasa.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, ilifafanua kuwa kufungwa kwa ubalozi wa China mjini Texas lengo lake ni kuhakikisha taifa hilo linalinda hakilimiliki ya wananchi wa Marekani.

“Tumeagiza kufungwa kwa ubalozi mdogo wa Jamuhuri ya watu wa China uliopo Houston, ili kulinda akilimiliki ya Wamarekani na taarifa za kibinafsi za Wamarekani”, alisema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Morgan Ortagus.

Ubalozi mdogo wa China wa Houston ni moja ya balozi ndogo tano za China zilizopo nchini Marekani, bila kuhesabu ubalozi wake uliopo Washington DC. Haijawa wazi kuhusu iwapo ubalozi huu pia umetajwa miongoni mwa zile zilizoamrishwa kufungwa.

Ortagus aliongeza kuwa Marekani “haitavumilia ukiukaji wa hadhi ya nchi yetu na vitisho vya Jamuhuri ya Watu wa China na kama tu ambavyo hatukuvumilia, utendaji wa biashara usio wa haki wa haki, wizi wa kazi za Wamarekani na tabia nyingine za uchokozi “.

Ortagus pia alitaja makubaliano ya Vienna kuhusu mahusiano ya kidiplomasia, ambayo yanasema nchi zina wajibu wa kutoingiliana kuhusu masuala ya ndani ya nchi mwenyeji.

Katika taarifa tofauti, wizara ya mambo ya nje ya Marekani iliishutumu China kwa kuhusika katika ujasusi mkubwa kinyume cha sheria na kushawishi utendaji, kuingilia siasa za ndani pamoja na kuwatisha wafanyabiashara wakuu, kuzitisha familia za Wamarekani wanaoishi China na tuhuma nyingine zaidi.

China ilitaja uamuzi huo uliochukuliwa na Marekani wa kuufunga ubalozi wake ni kama uchokozi wa kisiasa na kuongeza kueleza kuwa unakiuka sheria ya kimataifa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya China, Wang Wenbin alisema kuwa uamuzi huo ni wa kushitua na usio na sababu ya msingi na kwamba kilichofanyika ni kinyume na sheria za kimataifa.

Wang aliendelea kusema kwamba Washington imekuwa ikiilaumu China kupitia unyanyapaa na kuishambulia mara kwa mara. Aliitaka Marekani kufikiria, akisema kuwa iwapo itasisitiza kufuata mkondo huo wa mbaya, China italipiza kwa kuchukua hatua kali zaidi.

“Ukweli ni kwamba, kutokana na idadi ya balozi za China na Marekani pamoja na idadi ya balozi ndogo katika mataifa hayo mawili pamoja na idadi ya wafanyakazi katika balozi hizo, Marekani ina wafanyakazi wengi zaidi wanaofanya kazi nchini China”, alisema Wang.

Baadaye wizara ya masuala ya kigeni ilichapisha onyo kwa wanafunzi wa China nchini Marekani, ikiwataka kuwa macho kwa kuwa vitengo vya usalama nchini Marekani vimeanza kuwahoji, kuwanyanyasa na kuwapokonya mali zao wanafunzi wa China wanaosomea nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa mpya iliyotolewa na serikali ya China hatimaye nayo imejibu mapigo kwa kuchukua hatua kama zilizochukuliwa na Marekani.

Serikali ya China imechukua hatua ya kulipiza kisasi kwa Marekani kwa kuamuru kufungwa ubalozi mdogo wa nchi hiyo ulioko katika mji wa Chengdu kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Wizara ya mambo ya nje ya China imetangaza leo kuwa, imefuta kibali cha kazi kwa ubalozi mdogo wa Marekani ulioko katika mji wa Chengdu na kwamba hatua hiyo imechukuliwa kujibu mapigo kwa kitendo cha Marekani cha kuufunga ubalozi mdogo wa China katika mji wa Houston.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya China imefafanua kuwa hatua hiyo ni jibu halali kisheria na imehitajika kuchukuliwa kutokana na hatua za kimabavu na zisizo za kimantiki za Marekani.

Wizara hiyo ikaongeza katika taarifa yake na kwamba rais Marekani Donald Trump ndiye anayebeba dhima ya hatua zote hizo za mwenendo huo mbaya na ukiukaji ahadi.

Ubaozi mdogo wa Marekani katika mji wa Chengdu una wafanyakazi wapatao 200. Katika siku za hivi karibuni mivutano na mikwaruzano kati ya Marekani na China imeongezeka kutokana na sera za ubinafsi, ubabe na utumiaji mabavu zinazodaiwa kufanywa na Washington.

Utawala wa rais Donald Trump umekuwa na sintofahamu ya mara kwa mara na ule wa Beijing juu ya biashara na janga la virusi vya corona, pamoja na hatua ya China kuweka sheria mpya ya usalama juu ya Hong Kong.

Hivi karibuni wizara ya sheria ya Marekani iliishutumu China kwa kudhamini wadukuzi ambao wamekuwa wakilenga maabara zinazotengeneza chanjo za Covid-19.