BEIJING,CHINA

UBALOZI  wa China nchini Kazakhstan umetoa indhari juu ya mripuko wa homa ya mapafu isiyojulikana (pneumonia)  ambayo ni hatari zaidi kuliko ugonjwa wa Covid-19.

Ubalozi huo uliwaonya raia wake walioko nchini Kazakhstan na kusema kuwa, idadi ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo ni kubwa zaidi ya vifo vya corona.

Huku ubalozi wa China nchini Kazakhstan ukiutaja ugonjwa huo kama nimonia isiyojulikana, serikali ya Kazakhstan inasititiza kuwa maradhi hayo ni homa ya mapafu ya kawaida.

Ubalozi huo nchini Kazakhstan ulisema kasi ya maambukizo ya ugonjwa huo iliongezeka sana mwezi uliopita wa Juni, na kwamba hadi sasa kesi 500 ziliripotiwa katika maeneo matatu ya nchi hiyo, huku wagonjwa 30 wakiwa katika hali mahututi.

Kwa mujibu wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef),homa ya mapafu (pneumonia) inaua mtoto mmoja katika kila sekunde 39, na kwamba ugonjwa huo uliua watoto laki nane mwaka juzi pekee kote duniani.

Unicef inasema nusu ya vifo hivyo laki nane vya watoto kutokana na ugonjwa wa pneumonia viliripotiwa katika nchi za Nigeria, India, Pakistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ethiopia, na kwamba vifo hivyo viliwakumba watoto walio chini ya umri wa miaka miwili.

Licha ya kuwepo chanjo ya ugonjwa huo, lakini katika kila watoto 1000 walio chini ya miaka mitano, 90 huaga dunia kutokana na nimonia katika nchi za Angola, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Mali, Nigeria, Sierra Leone na Somalia.