NA ABOUD MAHMOUD
KLABU ya soka ya Chipukizi United imesema maamuzi yaliotolewa na kamati ya kusikiliza malalamiko ya awali ya ZFF hayakuwa sahihi na hawayakubali.
Akizungumza na Zanzibar Leo kocha mkuu wa klabu hiyo Mzee Ali Abdalla alisema maamuzi hayo ya kuipokonya pointi tatu na mabao mawili timu hiyo, hawakubaliani na hilo,
na hatua kali watazichukua.
“Hatukubaliani na maamuzi hayo sisi tunajua kama hii taarifa ya upotoshaji,”alisema.
Mzee alisema maamuzi hayo yaliotolewa kwa njia ya barua ambayo imewekwa kwenye mitandao ya kijamii ni batili, kwani hawajapokea barua ya malalamiko kutoka kwa kamati hiyo ya ZFF.
“Hiki walichokifanya mimi nakiita ni kitendo cha udhalilishaji kwa timu hii yenye historia nzuri ya soka Zanzibar, kwa sababu mechi wanayoilalamikia wenzetu wa Machomane kuchezesha wachezaji ambao hawana kibali sio kweli na ya muda mrefu, “alisema.
Kocha huyo alieleza walicheza mechi na Machomane Febuari 23 mwaka huu na ilikua ndani ya mzunguko wa pili wa ligi .
Alisema kwa majibu wa sheria ya kuendesha ligi ibara ya 23-15 inayoeleza malalamiko yoyote yasikilizwe si zaidi ya wiki moja, lakini alisema kamati hiyo aliyoiita ya mtu mmoja haikufuata kanuni hiyo na kuonesha kwamba haina maadili.
Alifahamisha katika mechi hiyo ambayo walitoka sare bila ya kufungana uwanja wa Gombani, wachezaji waliolalamikiwa ni Salum Suleiman Salum ambae wamemlipia kibali kinachoruhusu kucheza visiwani humu kutoka wilaya ya Ilala sambamba na mwenzake Shaali Hassan Ramadhan aliyetoka timu ya Cossovo na amelipiwa ngazi ya mkoa 50000/=.
Hivyo Mzee ameiomba ZFF kumchukulia hatua kali za kinidhamu viongozi waliohusika na upotoshaji wa taarifa kwa wapenda soka na serikali kwa ujumla.
Kocha huyo alisema kweli timu yake imeshuka daraja lakini haiko tayari kufanywa ngazi ya kupandia timu nyengine.
Tayari timu hiyo imeondoka jana asubuhi kuelekea kisiwani Pemba na kushindwa kucheza mchezo wake mmoja dhidi ya Polisi, ambapo Polisi ilipewa pointi za bure.
Akizungumzia sababu za kuondoka na kushindwa kucheza mchezo huo Mzee alisema, wameamua kuondoka baada ya kupata taarifa kuwa michezo ya ligi imesimamishwa kutokana na kifo cha rais mstahafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa.
Hata hivyo alisema jambo la kushangaza Jumamosi majira ya saa 4 usiku walipata taarifa za kuendelea kwa ligi hiyo, huku tayari ikiwa imewaruhusu wachezaji wake kuondoka kambini kwa ajili ya safari.