NA MWANDISHI WETU
HATIMAE serikali imekiunganisha rasmi Chuo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma Zanzibar (ZJMMC) na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kuanzia jana baada ya hatua hiyo kusubiriwa kwa muda mrefu.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wajumbe wa Baraza la tisa la Wawakilishi Zanzibar, kufuta sheria namba 11 ya 2006 ambayo ilianzisha chuo hicho na kutunga sheria mpya iliyotoa fursa kwa vyuo hivyo kuunganishwa.
ZJMMC sasa itakuwa moja ya Idara katika Skuli ya Kompyuta, Mawasiliano na Mafunzo ya Habari (SCCMS) ya chuo kikuu hicho ambapo kinachosubiriwa sasa ni kuidhinishwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, wa kwanza (kulia) akikabidhi hati za Chuo cha Uandishi wa Habari (ZJMC), kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Idrissa Muslim Hija, (katikati) na waziri wa Wizara hiyo Riziki Pembe Juma, baada kuunganishwa na Chuo Kikuu cha Zanzibar. (PICHA NA ABDALLA MASANGU).
Taasisi zingine zilizounganishwa na chuo kikuu hicho ni kilichokuwa Chuo cha Utalii Maruhubi, Chuo cha Kilimo Kizimbani, Chuo cha Afya Mbweni na Chuo cha Utawala wa Fedha, Chwaka.
Akikabidhi chuo hicho kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, alisema imani yake kuwa ZJMMC kitaendelea kuwa mikono salama.
Aliwasihi wafanyakazi wa ZJMMC kupunguza hofu juu ya ajira zao, akisema kuwa wale watakaokosa sifa ya kubakia SUZA watahamishiwa katika taasisi nyengine za serikali.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma, alisema kuunganishwa kwa chuo hicho ni mojawapo ya mkakati wa serikali wa kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Kutokana na hatua hiyo, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) sasa kitakuwa na kampasi saba ikiwemo ya Vuga, Beit Ras (Nkrumah), Benjamin Mkapa Pemba, Chwaka, Mbweni, Kizimbani, Tunguu na Kilimani.