WASHINGTON,MAREKANI

IDADI ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini Marekani imeongezeka kwa kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa baada ya watu wengine 50,000 kuambukizwa virusi hivyo ndani ya muda wa siku moja.

Maambukizo ya virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 yakiongezeka katika majimbo 40 kati ya 50 ya nchi hiyo.

Ilielezwa kuwa kutovaa barakoa au kutofuata maagizo ya kukaliana mbali kumechangia ongezeko hilo la maambukizo ya corona nchini humo.

Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, kesi mpya 50,700 za watu waliothibitika kuambukizwa virusi vya corona zilisajiliwa kikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuliko hata kile ambacho nchi hiyo ilishuhudia katika kipindi hatari zaidi cha maambukizo mnamo miezi ya Aprili na Mei.

Marekani iliripoti kuwa watu wasiopungua milioni mbili na laki saba waliambukizwa virusi vya corona na zaidi ya 128,000 walifariki dunia hadi sasa, kikiwa ni kiwango cha juu zaidi duniani. 

Takwimu za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins aidha zinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni kumi na laki saba walithibitika kuugua ugonjwa wa Covid-19 duniani kote ambapo idadi ya vifo vilivyosababishwa na ugonjwa huo hadi sasa imeshapindukia 516,000.