ABUJA,NIGERIA

WATU  milioni 50 katika nchi za Afrika wametumbukia katika lindi la umaskini kutokana na makali ya janga la corona.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB),ambayo ilibainisha kuwa,maeneo ya magharibi na katikati mwa bara hilo ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na mdororo wa uchumi uliosababishwa na janga la ugonjwa wa Covid-19.

Aidha taasisi hiyo ya kifedha ilisema huenda watu kati ya milioni 24.6 na 30 barani humo wakapoteza nafasi zao za ajira mwaka huu 2020, kutokana na janga la corona.

Takwimu za Benki ya Maendeleo Afrika zinakadiria kuwa, karibu thuluthi moja ya wakaazi wote wa bara hilo wataishi chini ya mstari wa kimataifa wa umaskini wa dola 1.90 kwa siku mwaka huu 2020.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alisema  kusambaa virusi vya corona barani Afrika kutawafanya mamilioni ya watu wa bara hilo kukumbwa na umasikini mkubwa na baa la njaa.

Mapema mwezi huu wa Julai,Kamishna wa Miundombinu na Nishati wa Umoja wa Afrika AU alisema kuwa, nchi za bara hilo zilipata hasara ya dola bilioni 55 za ushuru wa usafiri na utalii katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kutokana na ugonjwa hatari wa COVID-19.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani, idadi ya kesi za ugonjwa wa Covid-19 (corona) zilizothibitishwa katika nchi za Afrika ni zaidi ya laki tano, huku idadi ya vifo vilivyosababishwa na maradhi hayo barani humo ikiwa ni zaidi ya 12,000.

Hata hivyo wagonjwa zaidi ya laki mbili na elfu 53 wa corona wamepata afueni barani humo.