NA MWANAJUMA MMANGA

KUIBUKA kwa maradhi ya Corona kumezorotesha maendeleo ya ujenzi wa mradi wa soko jipya la Samaki Malindi ulioanza mwezi Mei 2019.

Mratibu wa mradi huo, Daudi Haji Pandu kutoka Wizara ya Kilimo Maliasili, Mifugo na Uvuvi, aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa njia ya simu.

Alisema hadi sasa mradi huo umefikia hatua ya ukamilishaji wa ujenzi wa maegesho ya vyombo vya uvuvi baharini.

Alisema pamoja na changamoto hiyo iliyojitokeza lakini mradi huo umefikia hatua kubwa na nzuri ili kukamika kwake.

Aidha alisema wanachokisubiri hivi sasa ni kumsubiri mfadhili wa mradi huo ambae ni taasisi ya JECA kutoka Japan kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huo.

“Mradi huo hapo mwanzo tulitarajia utakamika  mwezi Mei 2021 ambao ni mradi ulitegemewa kuchukua miaka mitatu kuanzia mwanzo wa Mwezi 2019” alisema

Alisema kazi itayofuata ni ujenzi  wa  bandari ya uvuvi  ya kisasa  (diko)  ambayo  itahudumia  boti mbali mbali  za  wavuvi wa Zanzibar.