TEHRAN,IRAN

JAMHURI  ya Kiislamu ya Iran inatarajia kuanza kusambaza masokoni dawa ya kupambana na virusi ya ‘Remdesivir’ iliyozalishwa nchini humo.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya na Elimu ya Utabibu wa Iran, Dakta Saeed Namaki na kubainisha kuwa, dawa ya kupambana na virusi ya Remdesivir iliyozalishwa nchini itaingia masokoni wiki ijayo.

Hakuna dawa yenye kutegemewa iliyoidhinishwa rasmi na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa Covid-19, lakini dawa hii ya Remdesivir na ile ya Favipiravir zilipendekezwa na baadhi ya madaktari kwa ajili ya kutibu wagonjwa wa Covid-19, baada ya kuonyesha matokeo mazuri katika nchi mbali mbali duniani haswa Marekani na Ulaya.

Mwishoni mwa mwezi uliopita pia, Waziri wa Afya wa Iran alitangaza kuwa wanasayansi wa humu nchini wapo mbioni kuanza kuzalisha chanjo ya ugonjwa wa Covid-19, na kwamba tayari chanjo hiyo ilishafanyiwa majaribio kwa wanyama kwa mafanikio, hatua ambayo iliongeza matumaini ya kudhibitiwa kikamilifu janga la corona duniani.

Wizara ya Afya ya Russia ilitangaza kwamba ilisajili dawa nyengine iliyopewa jina la ‘Levilimab’ kwa ajili ya kutibu wagonjwa mahututi wa corona, siku chache baada ya nchi hiyo kuzindua dawa nyengine ya kutibu waathirika wa Covid-19 ya ‘Avifavir.’ Hivi sasa nchi mbali mbali duniani ikiwemo Afrika Kusini zinafanyia majaribio dawa aina ya Dexamethasone yenye uwezo wa kuepusha hatari ya kifo miongoni mwa wagonjwa mahututi wa Covid-19, iliyogunduliwa na watafiti katika Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza.