Na Masanja Mabula ,PEMBA

SHIRIKA la Direct Aid limezikabidhi familia tano za kisiwa cha Fundo wilaya ya Wete  Mkoa wa Kaskazini Pemba vifaa vya uvuvi vyenye thamani ya shilingi milioni 18, ikijumuisha boti, mashine, mitengo  na life jaketi.

Akikabidhi vifaa hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba,   Omar Khamis Othman, alizitaka familia zilizopewa kuhakikisha vinatumika kama ilivyokusudiwa na kuahidi kutosita kuchukua hatua kisheria ikiwa ni pamoja na kuvikamata iwapo vifaa hivyo vitatumika kinyume na ilivyokusudiwa.

“Haitakuwa jambo jema chombo nimekikabidhi mimi baadaya nikamate kutokana na kukiuka sheria , lakini sina budi nitafanya hivyo iwapo kitafanya kazi ambazo hazikukusudiwa”alisisitiza.

 Mapema Mkurugenzi  wa Shirika hilo, Aliy Adam Aliy, alisema vifaa hivyo ni vya familia tano, na haitakuwa vizuri akatokea mmoja na kudai ni mali yake na kuvitumia kwa maslahi yake, kwani vifaa hivyo vinaweza kuongeza kipato cha familia hizi, iwapo watavitumia kwa ajili ya shughuli za kujiletea maendeleo.