WanaCCM wamsubiri kwa hamu
NA KHAMISUU ABDALLAH
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa kumtambulisha mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Dk. Hussein Mwinyi kisiwani Pemba.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Tibirinzi majira ya 8:00 mchana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Akizungumza na Zanzibar Leo kwa njia ya simu, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao alisema mgombea huyo atawasili katika uwanja wa Ndege kisiwani Pemba majira ya saa 4:00 asubuhi na kupokelewa na viongozi, wanaCCM na wananchi wa kisiwa hicho.
Alisema, mgombea huyo mara baada ya kupokelewa katika kiwanja hicho atapita katika barabara ya Madungu hadi Tibirinzi kwa ajili ya kuzungumza na wananchi na wanaCCM.
Alisema, katika mapokezi hayo kutakuwa na shamrashamra mbalimbali ikiwemo ngoma za asili na wasanii watakaonogesha mkutano huo. “Kila tunapopita watu tumeona wamehamasika kwa kupamba rangi ya kijani na njano kumsubiri kwa hamu mgombea wao”, alisema.
Hivyo, aliwasisitiza wananchi kisiwani Pemba kujitokeza kwa wingi katika mapokezi hayo na mkutano wa kutambulishwa mgombea huyo ambao atapewa fursa ya kuzungumza na wananchi na wanaCCM wa kisiwa hicho dhamira yake kwa wananchi wa Zanzibar.
“Wapenzi wa Pemba nawaomba msipitwe katika mapokezi haya kwani tuliona Unguja mapokezi kwani kesho ni siku yetu wapenda amani na maendeleo ili kumpokea mgombea wetu ambaye chama kimetuletea wazanzibari,” alibainisha.
Mapokezi kama hayo kwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi Unguja yalifanyika Julai 15 na baadae kuwahutubia wananchi na wanaCCM katika ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi aliteuliwa Julai 10 mwaka huu na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa baada ya kupata kura 129 sawa na asilimia 78.8 na kupewa baraka na mkutano mkuu wa CCM.