NA SAIDA ISSA, DODOMA
MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, amesema atatumia staili ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kuiongoza Zanzibar.
Dk. Mwinyi alieleza hayo jana alipopewa fursa ya kuzungumza kwenye mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete uliopo Dodoma.
Mgombea huyo aliyepitishwa juzi na halmashauri kuu ya CCM, alisema wapo watu wanamuona mpole na kudhani kuwa atashindwa kuiongoza Zanzibar kwamba dhana zao hizo ni potofu.
“Nitatumia staili ya Rais John Pombe Magufuli katika kupambana na rushwa na uzembe na kwamba nitakuwa mkali sana kwenye mambo hayo,” alisema.
Katika hotuba yake hiyo fupi, alisema katika maisha yake ya uongozi amejifunza mengi katika kipindi cha miaka mitano ya Dk. John Pombe Magufuli.
Alitumia fursa hiyo kuwaeleza wanaCCM kwamba wagombea wote waliojitokeza kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia CCM ni marafiki na hawana tofauti baina yao.
“Wenzangu niliogombea nao wote wamenihakikishia kupata ushirikiano wao sisi ni marafiki, hatuna makundi, hivyo tuvunje kambi zetu,”alisema.
Alisema ili CCM iweze kushinda kwenye uchaguzi mkuu ni muhimu kuwepo ushirikiano na kwamba kambi zote zitavunjwa na kuwa na kambi moja kubwa itakayoitwa CCM ambayo ndiyo itakayoleta ushindi.
Dk. Mwinyi alimshukuru Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa akimtaja kama mtu aliyemfungulia milango kwenye safari yake ya kisiasa.
Alisema akiwa na miaka 33, mzee Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Afya akiwa mbunge wa jimbo la Mkuranga na hata alipounda taasisi yake ya ‘Mkapa Foundation’ inayopambana na ugonjwa wa UKIMWI alimuomba amsaidie.
Aidha alimpongeza Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kumuamini na kumteuwa kuwa waziri na kumpongeza Dk. Shein ambaye alifanyakazi naye akiwa waziri wa muungano.
Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo pia kumpongeza mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye ni baba na mama yake mama Siti Mwinyi pamoja na familia yake.