NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, jana alikuwa ni miongoni mwa wajumbe wa mkutano mkuu waliopiga kura ya maoni kumchagua mbunge na mwakilishi wa jimbo la Tunguu.

Zoezi hilo limefanyika huko katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo kampasi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), huko Tunguu wilaya ya kati mkoa wa Kusini Unguja.

Makamu Mwenyekiti huyo akiwa miongoni mwa wajumbe hao alishiriki  katika zoezi hilo la kuwachagua viongozi hao wa jimbo la Tunguu akiwa ni miongoni mwa wajumbe 160 waliohudhuria kati ya wajumbe wote 176 wa jimbo hilo.

Zoezi hilo lilikuwa na jumla ya wagombea wa nafasi ya ubunge ambao jumla yao walikuwa kumi na wagombea nafasi ya uwakilishi jumla yao walikuwa ni 14 ambao mapema walipata fursa ya kujielezea na kunadi sera zao mbele ya wajumbe hao wa mkutano mkuu wa jimbo hilo.

Mapema Mwenyekiti wa CCM jimbo la Tunguu, Ramadhan Khatib Ramadhan aliwasihi wajumbe wa mkutano huo kuwa zoezi hilo ni utaratibu uliowekwa na CCM kila ifikapo miaka mitano ya uchaguzi.

Alisema kuwa utaratibu huo ni kwa mujibu wa sheria na katiba ya CCM ambao unakiongoza chama hicho.

Aliwataka wagombea wote wa nafasi hizo kukubali na kuridhika na matokeo watakayoyapata kwani waliogombea nafasi hizo ni wengi, lakini wanaohitajika ni mmoja kwa nafasi ya uwakilishi na mmoja kwa nafasi ya ubunge.

Mwenyekiti huyo wa CCM alisisitiza haja ya kuwachagua viongozi wenye sifa na uwezo wa kukitetea chama hicho na kukitumikia kwa moyo wao wote kutokana na chama hicho kuimarika kwa muda mrefu tokea kuasisiwa Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Pamoja na hayo, kiongozi huyo aliwaeleza wajumbe na wagombea nafasi hizo kwamba uchaguzi huo utakuwa huru na haki kwa kufuata miongozo yote ya CCM sambamba na katiba, sheria na kanuni.