Kutambulishwa mbele ya umati
Mapokezi ya kishindo yamsubiri
NA MADINA ISSA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein atawaongoza wanaCCM na wananchi visiwani hapa kwenye hafla rasmi ya mapokezi kwa mgombea wa chama hicho kwenye uchaguzi ujao, Dk. Hussein Mwinyi.
Wanachama wa chama hicho hapa Zanzibar, wamekuwa wakimsubiri kwa hamu na shauku mgombea wao huyo ambaye Julai 10 mwaka huu, alichaguliwa na halmashauri kuu ya CCM taifa kugombea nafasi hiyo.
Halmashauri kuu ya CCM taifa iliyokutana katika ukumbi wa mikutano wa chama hicho ‘White House’ jijini Dodoma, ilimchagua Dk. Hussein Mwinyi kwa ushindi wa asilimia 78.6 na kuwashinda Dk. Khalid Salum Mohammed aliyepata asilimia 11.5 na Shamsi Vuai Nahodha aliyepata asilimia 9.7.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chama cha Mapinduzi, ilieleza kuwa Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ataongoza hafla ya kutambulishwa kwa Dk. Mwinyi ikiwa ni mara ya kwanza kuja Zanzibar tangu achaguliwe kuwa mgombea wa CCM.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, alisema hafla hiyo itahudhuriwa na wanachama kutoka mikoa mbalimbali ya Zanzibar.
Alisema kuwa baada ya kufika katika ofisi za chama mgombea huyo atazuru kaburi la aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu mzee Abeid Amani Karume na kuweka saini kitabu cha wageni.
Katibu huyo, alifahamisha kuwa Dk. Mwinyi atapata fursa ya kuzungumza na wazee wa CCM katika ukumbi wa mkutano uliopo katika ofisi hizo na kuzungumza na wanaCCM waliofika kumpokea.
Alisema maandalizi yameshakamilika kwa asilimia 100 ambapo kinachosubiriwa ni wanachama kumpokea mgombea huyo wa urais, na mapokezi yanatarajiwa kuanza majira ya mchana katika ofisi za chama Kisiwandui.
Alisema mgombea baada ya kuwasili katika kiwanja cha ndege, msafara wake utaanzia Kiembesamaki, Mazizini, Migombani, Kilimani, Magereza, Kariakoo, Mwembekisonge, hadi ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.