NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa aliyahifadhi na kuyalida Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwa vitendo.

Dk. Shein aliongeza kuwa mzee Mkapa aliuhifadhi na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa vitendo, hivyo ataendelea kuheshimiwa kwa uzalendo wake huo.

Aliyasema hayo wakati akitoa salamu za wananchi wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufuatia kifo cha marehemu Benjamin Mkapa katika maziko yaliyofanyika huko kijijini kwake Lupaso, Mkoa wa Mtwara, Wilaya ya Masasi.

Alisema wananchi wataendelea kumuenzi na kumkumbuka rais mstaafu Mkapa katika maisha yao yote sambamba na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu.

Dk. Shein alisema kuwa kwa majonzi makubwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wa Mkoa wa Mtwara na hasa wilaya hiyo ya Masasi katika maombolezo ya msiba huo mkubwa.

Aidha, alimtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Joseph Magufuli kupokea salamu hizo za wananchi wa Zanzibar huku akisisitiza kwamba mauti ni safari ya lazima kwa kila mwanaadamu.

Nao marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nyakati tofauti walitoa salamu zao za mwisho kabla ya kuzikwa kwa Rais Mkapa na walitumia fursa hiyo kumuelezea Rais Mkapa jinsi walivyomfahamu kwa miaka mingi sambamba na utekelezaji wake wa kazi.

Kikwete kwa upande wake alieleza kuwa Marehemu Mkapa alikuwa ni kiongozi mtambuzi wa manufaa ya watu wake anaowaongoza ambaye amelifanyia mengi taifa hili la Tanzania katika uongozi wake.

Mzee Mwinyi alisema kuwa Rais Mkapa alikuwa ni mtu mzuri sana, mwema sana na mbaridi sana lakini alikuwa ni mfanya kazi kweli kweli na alikuwa hana masihara katika kazi mambo ambayo yameleta manufaa kwa Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwashukuru viongozi wote na wananchi pamoja na kamati ya Kitaifa iliyoshughulikia vyema msiba huo huku akimuelezea rais Mkapa kuwa alipenda kwao na kuwataka Watanzania kujifunza jambo hilo kwani Mzee Mkapa aliusia kuzikwa katika kijiji alichozaliwa cha Lupaso.

Nao wanafamilia wa marehemu mzee Mkapa walitoa shukurani kwa wananchi na viongozi wote pamoja na Serikali kwa kuujali na kuushughulikia msiba wa Rais Mkapa ambapo maziko ya kiongozi huyo yalifanyika kwa taratibu zote za Kiserikali na kidini.