NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa mkono wa pole kwa familia ya rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa na kueleza kuwa kiongozi huyo atakumbukwa kwa mambo mazuri aliyoifanyia Tanzania.
Dk. Shein alifika nyumbani kwa marehemu mzee Mkapa majira ya saa tano za asubuhi katika mtaa wa Masaki jijini Dar es Salaam ambapo alitoa mkono wa pole kwa familia na mjane wa marehemu mama Anna Mkapa.
Mara tu baada ya kufika nyumbani kwa marehemu Dk. Shein alitia saini kitabu cha maombolezo na huku akimuomba Mwenyezi Mungu aipe subira familia ya mzee Mkapa katika kipindi hichi kigumu cha msiba.
Baada ya matukio hayo, Dk. Shein alipata fursa ya kufanya mahojiano na waandishi wa habari ambapo alimuelezea mzee Mkapa kuwa ni kiongozi mahiri aliyefanya kazi nae kwa muda wa miaka minne na nusu na kujifunza mambo mengi.
Dk. Shein alieleza kuwa Mkapa aliifikisha Tanzania mahala pazuri sana kwa kusimamia misingi ya uchumi ambayo hatimae ilisaidia Tanzania kuimarika kiuchumi.
Aliongeza kuwa mzee Mkapa ameitumikia nchi kwa nidhamu kubwa sana ikiwa ni pamoja na kusimamia nchi kiuchumi na kimaendeleo sambamba na kuisimamia nchi kwa misingi yote ya amani na utulivu mkubwa.
Alisema kuwa msiba huo ni wa watanzania wote na kwa kila anaependa maendeleo wa ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akisisitiza kumuombea ili apumzike kwa salama.
Katika kufuata misingi ya Mkapa, Dk. Shein aliwataka viongozi waliopo madarakani wazee na vijana kujifunza uongozi kutoka kwa Mkapa kwani kiongozi huyo ni mtu aliyeishi vizuri na watu wa maeneo yote tena bila ya kuwabagua.
Dk. Shein alieleza kuwa anayakumbuka mengi aliyoyafanya Mkapa wakati anafanya kazi nae pamoja ikiwa ni pamoja na kusaidia sana kuibadilisha nchi kwa kufanya mabadiliko ya kiuchumi sambamba na kuimarisha utawala bora kwa kuanzisha Wizara ya Utawala Bora ambayo ilikuwa ndiyo Wizara ya mwanzo katika Serikali za nchi za bara la Afrika huku akisimamia kwa vitendo uchumi wa Tanzania.
Alisema kuwa wakati mzee Mkapa anaingia madarakani makusanyo yalikuwa madogo wastani wa shilingi bilioni 1.7 mnamo mwaka 2005, lakini kutokana na juhudi zake makusanyo yaliimarika zaidi hatua ambayo pia ilipelekea kufanyika kwa mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Alieleza kuwa kubwa kabisa na la muhimu alilofanya mzee Mkapa ni kusimamia mwenendo mzuri wa uchumi wa nchi kwani hilo linatokana na uzoefu wake wa uongozi kwani awali aliwahi kuwa waziri katika wizara kadhaa za Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Kutokana na Mkapa kumtaja Dk. Shein katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose” Rais Dk. Shein alisema kuwa ameweza kumtaja katika kitabu chake hicho kwani alifanya kazi nae na kuishi nae vizuri kwani akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Shein alifanya kazi na marehemu Mkapa na kumheshimu na kumuweka kuwa ni kiongozi wake, mkubwa wake na pia, alikuwa ni kiongozi wake wa Chama.
Dk. Shein alieleza kuwa yeye kwake ilikuwa ni rahisi sana kufanya kazi na mzee Mkapa kwani ni mkubwa wake na pia ni kiongozi wake wa kazi hivyo, alifanya kazi kwa kumheshimu na kuishi nae vizuri na kumuacha afanye kazi zake bila ya kumuingilia hiyo ni kutokana na kumuamini wakati wote.
Dk. Shein alisema kuwa hatua yake hiyo ilimpelekea kufanya kazi kwa kujiamini na kusisitiza kuwa ni mtu ambaye ukifanya kazi nae unaona raha sana kwani anakuachia kufanya kazi zako vizuri kwani ni mtu aliyekuwa akishaurika na ni mtu aliyekuwa akielekeza namna ya kufanya kazi kwani alikuwa mtu wa mfano wake.