NAIROBI,KENYA
BARAZA la Biashara la nchi za Afrika Mashariki (EABC), limezitaka nchi zote za kanda hiyo kufuata mfano wa Tanzania kwa kufungua anga zao ili kuruhusu safari za kimataifa kuingia na kutoka katika kanda hiyo.
Taarifa iliyotolewa na baraza hilo ilisema ingawa wizara katika nchi hizo zina haki ya kuchukua hatua kuhakikisha kuwa maambukizi ya Virusi vya Corona yanapungua, lakini umefikia wakati anga zote zifunguliwe kwa ajili ya kufungua biashara na shughuli za kitalii katika mataifa ya Afrika Mashariki.
“Kufunguliwa kwa anga kutasaidia kuimarisha sekta ya usafiri wa anga ambapo sekta ya utalii inategemea kwa kiasi kikubwa usafiri huo,”taarifa hiyo ilisema.
Tayari mataifa ya Kenya na Rwanda yameshafungua anga zao kwa ajili ya usafiri wa ndani ambapo Rwanda ilifungua tangu Juni 18 na Kenya inatarajia kufungua usafiri wa anga wiki hii kwa safari za nyumbani.
Safari za kimataifa ambazo kwa kiasi kikubwa zinategemewa sana kuingiza watalii wengi katika kanda ya Afrika Mashariki, zinatarajiwa kuanza rasmi tarehe Mosi Agosti mwaka huu katika mataifa ya Kenya na Rwanda.
Kwa upande wa mataifa ya Uganda na Burundi, baraza hilo linaendelea kushauriana na nchi hizo ili kuhakikisha kuwa yanafungua anga zao kama ilivyo kwa wenzao wa Tanzania, Kenya na Rwanda.
Uganda iliunga mkono pendekezo la kufungua anga kwa ajili ya kuokoa sekta ya utalii katika taifa hilo iliyoharibiwa na janga la virusi vya corona.