KAMPALA,UGANDA

MAHAKAMA  ya Uadilifu ya Afrika Mashariki EACJ imeanza kusikiliza kesi ya kupinga uamuzi wa Mahakama juu ya Uganda, ya kuidhinisha mabadiliko ya katiba yalioondoa ukomo wa umri wa kugombea urais katika nchi hiyo, wa miaka 75.

Mahakama hiyo yenye makao yake mjini Arusha nchini Tanzania ilianza kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya intaneti, ili kufuata protokali za afya za kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Kesi hiyo iliwasilishwa katika mahakama hiyo ya kikanda na wakili mashuhuri wa Uganda, Male Mabirizi.

Faili hilo la Mabirizi linasikilizwa na jaji wa Uganda, Monica Mugenyi ambaye ni Jaji Mwandamizi wa Mahakama hiyo , akishirikiana na majaji wengine Charles Nyawello na Charles Nyachae.

Awali kesi hiyo ilikuwa imeratibiwa kusikilizwa kuanzia Machi 18 hadi 30 mwaka huu, lakini ratiba hiyo ikavurugwa na janga la corona.

Mwanasheria Mkuu wa Uganda, Mwesigwa Rukutana ambaye anapaswa kuiwakilisha serikali ya Kampala katika kesi hiyo, alikuwa akisisitiza kuwa, masuala yaliyoibuliwa na wakili Mabirizi katika kesi hiyo tayari yamepatiwa ufumbuzi na mahakama za Uganda. 

Uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Uganda wa Aprili mwaka jana 2019, ulioidhinisha marekebisho ya kuondoa kipengele kinachoweka ukomo wa umri wa miaka 75 kwa mgombea wa kiti cha urais, ulimpa Rais Yoweri Museveni ambaye aliiongoza Uganda tangu mwaka 1986 na mwenye umri wa miaka 75, nafasi ya kuwania tena kiti hicho mwaka 2021 na kuendelea hadi mwaka 2026.

Upinzani dhidi ya mabadiliko hayo ya sheria ulimuibua Mbunge chipukizi, Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’ ambaye kwa sasa  alikuwa kama kinara wa upinzani na mwiba mkali dhidi ya serikali ya Museveni ndani na nje ya bunge la nchi hiyo ya Afrika Mashariki.