KAMPALA,UGANDA
TUME ya Uchaguzi Uganda (EC),imeiomba mahakama itoe muda zaidi wa kupiga kura ili kuwawezesha wafungwa na raia wengine wa Uganda kushiriki katika Uchaguzi wa Kitaifa.
Maombi hayo ambayo yalifikishwa katika Mahakama Kuu, EC kupitia ofisa wake wa kisheria Hamid Lugoloobi alisema kuwa tume hiyo haina pesa za kuwezesha kukamilika mchakato huo kwa haraka.
Lugoloobi alisema kuwa pesa zilizotengwa kwa tume kwa mwaka wa fedha 2020/2021 zinaweza kushughulikia Waganda waliosajiliwa tu.
Mwezi uliopita, Jaji Lydia Mugambe, alifuta marufuku ya miaka 25 ya haki za kupiga kura ya wafungwa na Waganda nje ya nchi.
“Kama raia, Waganda wa miaka kumi na nane na zaidi ambao wako gerezani au Diaspora wana haki ya kupiga kura chini ya Kifungu cha 59 cha Katiba,” Jaji Mugambe aliagiza.
Lugoloobi katika hati yake alisema kuwa bila chanzo chengine cha ufadhili huru, janga la Covid-19, pamoja na muda uliowekwa wa miezi saba tu kwa uchaguzi, EC haiwezi kufungua daftari la wapiga kura na kujumuisha wafungwa na Waganda nje ya nchi.