BAMAKO, MALI

MKUTANO wa dharura wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) unatarajiwa kufanyika Jumatatu wiki ijayo kwa njia ya video kwa ajili ya kujadili na kuchukua hatua kuhusiana na mgogoro unaoikabili nchi ya Mali.

Mkutano huo unatafanyika baada ya marais watano kutoka nchi za ECOWAS kukutana Alkhamisi ya juzi Bamako na wadau mbalimbali wakiwemo Rais Ibrahim Boubakar Keita wa Mali, wawakilishi wa upinzani na mashirika ya kiraia kujaribu kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Mali.

Kiongozi upinzani nchini mali Imam Mahmoud Dicko, alisema hakuna hatua chanya yoyote iliyofikiwa katika mazungumzo ya jana na kwamba watu waliopoteza maisha hawawezi kuachwa roho zao zipotee bure.

Hivi karibuni wapinzani nchini Mali walikataa pendekezo la Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za magharibi mwa Afrika na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo kama njia ya kuhitimisha mgogoro unaoikabili nchi hiyo.

Awali Rais Keita alikuwa ameafiki pendekezo la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa, kufanyiwa mabadiliko mahakama kuu na kuvunjwa bunge lakini wapinzani wamekuwa wakisisitiza kuwa mabadiliko hayo hayatoshi na wanamtaka aondoke madarakani.

Kuanzia Juni 10 Mali imekuwa ikishuhudiwa maandamano makubwa dhidi ya Rais Keita ambapo waandamanaji wanasisitiza kuwa lazima aondoke madarakani.

Wapinzani walisema rais huyo amefeli katika utendaji kazi wake kuhusu mgogoro wa muda mrefu wa waasi, mgogoro wa kiuchumi na mvutano ulioibuka baada ya uchaguzi wa bunge mwaka jana.