KIFUA kikuu ni ugonjwa wa kuambukizwa ulio hatari sana ambapo ugonjwa huu husababishwa na aina mbalimbali za bakteria zinazojulikana kitaalamu Mycobacterium tuberculosis.

Kifua kikuu kwa kawaida kinaathiri mapafu, lakini pia kinaweza kuathiri sehemu nyingine za mwili.

Ugonjwa huu husambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa kupitia hewa wakati mgonjwa anapokohoa, kupiga chafya, au mate yake yakiwa hewani.

Kwa kawaida maambukizi mengi hayana dalili wala hayaleti madhara, lakini moja kati ya maambukizo kumi yasiyoleta madhara hatimaye huendelea na kuwa ugonjwa kamili.

Kama kifua kikuu kisipotibiwa, kinaua zaidi ya asilimia 50 ya watu walioambukizwa.

Dalili za kawaida za maambukizi ya kifua kikuu kinacholeta madhara ni kikohozi sugu na kukohoa damu, Kohozi, homa, kutokwa na jasho usiku, na kukonda. 

Ili mgonjwa alieugua kifua kikuu kupona ni lazima kupata tiba ya hospitali na si kutumia tiba asili au kwenda kwa waganga wa jadi.

Lakini cha kushangaza kumekuwa na taarifa za kushangaza kuwa baadhi ya watu wanaougua kifua kikuu huenda kwa waganga wa jadi ama kutumia mizimu au matambiko jambo ambalo halikubaliki kabisa kitabibu.

Tunasema hivyo tukifahamu kuwa wako baadhi ya watu wanaougua ugonjwa huo wamekuwa wakikimbilia kwenye tiba asili au kwa waganga wa jadi jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao na hata jamii inayowazunguka hasa ikizingatiwa kuwa ugonjwa huu unaambukiza.

Tunaamini kuwa bado jamii imekuwa na uelewa mdogo kujua dalili za ugonjwa huo, hivyo kusababisha kuchelewa kufika katika vituo vya afya sambamba na kujikita zaidi kwenye tiba asilia wakati wanapoona dalili hizo.

Hivyo, basi tunawaomba wananchi kuhakikisha kuwa wanapoona dalili kama hizo zilizotajwa ni vyema wakaenda kituo cha afya nasio kukimbilia kwenye tiba asili, jambo ambalo linahatarisha maisha ya wagonjwa.