WASHINGTON,MAREKANI

RIPOTA maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema Marekani imeiweka dunia katika hatari ambayo haijawahi kushuhudiwa kutokana na hatua ya jeshi lake kumuua Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda shahidi wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC).

Agnès Callamard alisema hayo jana wakati akikabidhi ripoti yake juu ya mauaji hayo ya kigaidi kwa Baraza la Haki za Binadamu la UN na kusisitiza kuwa, wakati umefika kwa jamii ya kimataifa kuvunja kimya chake juu ya mauaji ya kiholela yanayofanywa na Washington kwa kutumia ndege zisizo na rubani .

Callamard aliliambia Baraza la Haki za Binadamu la UN kuwa, mauaji hayo ya Januari 3 yaliweka kumbukumbu na mfano hatari, sambamba na kuiweka dunia katika ncha ya jabali.

Alitaja shambulizi hilo kama tukio la kwanza kuwahi kunakiliwa, ambapo dola limetaja ni kujihami kuhalalisha mauaji ya ofisa wa serikali nje ya eneo liiloshuhudia mgogoro wa kivita.

Kabla ya kukabidhi ripoti yake kwa Baraza la Haki za Binadamu la UN hapo jana,Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria alisema Marekani ilishindwa kutoa ushahidi wa kutosha wa kuyapa nguvu madai yake kwamba Jenerali Soleimani alikuwa tishio kwa taifa hilo.

Ofisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa anasisitiza kuwa, mauaji hayo ya kigaidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani yalikiuka sheria za kimataifa na Hati ya UN.