NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema ipo tayari kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu ambao utawaingiza madarakani viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya urais hadi majimbo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alisema serikali itaendesha uchaguzi kwa pesa zake wenyewe bila ya kusaidiwa.

“Serikali yenu wananchi ipo makini, Tume ya Uchaguzi itakapotangaza tarehe basi tutauendesha kwa pesa zetu wenyewe hatutaki kusaidiwa, wakija kwa mambo mengine tutawakaribisha lakini sio mambo ya uchaguzi ni jukumu letu wenyewe”, alisisitiza.

Dk. Shein ambae pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisema CCM imeshajiandaa kushindana uchaguzi wa mwaka huu kwani imeteua mgombea makini, muadilifu, mpenda amani na maendeleo.

“Anaetaka wembe umkate aje ashindane na sisi mwaka huu wembe wetu utakuwa mkali kuliko miaka iliyopita,” alisema.

Alisema, CCM imemchagua mgombea huyo kwani ni shabaha kubwa katika kuandaa mipango mizuri ya baadae kutekeleza ilani kwa kuitumikia na kuijenga Zanzibar.

“Kuchaguliwa kwake ni nguzo kubwa na ya msingi katika chama chetu na hali ya Zanzibar,” alisema.

Aidha, alibainisha kwamba CCM sio chama cha mchezo bali ni chama na wanaCCM wenyewe kwani wanakitunza kukilea na kukiendesha. “Hatuna shaka chini ya uongozi wako mambo yakianza tutashinda kwa kishindo”, alisema.  

Hivyo, aliwasisitiza wananchi na waCCM kushirikiana na kuwa na nguvu ya pamoja ili kuhakikisha CCM inaendelea kushinda katika uchaguzi wake kama zilivyo chaguzi nyengine zilizofanyika miaka ya nyuma.

Tayari Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imeshafanya mambo mbalimbali ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu ikiwemo uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa wapiga kura waliokuwemo katika daftari la kudumu.

Kazi nyengine ni kuweka mapitio ya idadi, mipaka na majina ya majimbo ya uchaguzi kwa mwaka huu, kuweka hadharani daftari la kudumu la wapiga kura na kuanza kwa zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya kupigia kura kwa wananchi wote waliojiandikisha katika daftari la kudumu.