Imelenga huduma za kijamii
NA TATU MAKAME
KATIKA kuleta maendeleo zaidi na madaraka mikoani, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa makusudi imeamua kuanzisha taasisi za serikali za mitaa yaani halmashauri za wilaya kwa lengo la kuzisogeza zaidi huduma kwa jamii.
Kwa mfano, halmashauri ni moja ya taasisi za serikali ambazo zinafanya kazi za kutoa huduma kama taasisi nyengine za umma na hasa katika ngazi za wilaya na za mikoa.
Kwa mujibu wa sheria nambari 7 ya mwaka 2014 serikali ya mitaa halmashauri zinafanya kazi ya kupeleka madaraka kwa wananchi.
Tangu kupelekwa madaraka kwa wananchi halmashauri zimeleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji ikiwemo kuongezeka kwa mapato kwa kila mwaka kutokana na utendaji wake wa kazi.
Katika makala haya tunazungumzia halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini ‘B’ juu ya utendaji wake kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Makame Mwadini Silima, akizungumza na makala haya alisema halmashauri hiyo yenye watendaji 980 wakiwemo wa mkataba 66 na wenye ajira za kudumu 914 imekuwa ni chachu kubwa ya maendeleo katika jamii inayozunguka eneo hilo.
Alisema halmashauri hiyo imebuni miradi ya maendeleo ambayo imepitishwa na mabaraza ya madiwani kupitia mawazo ya wananchi kuanzishwa miradi hiyo katika wadi zao na kutekelezwa na halmashauri kwa ushirikiano na mifuko ya majimbo kupitia wabunge na Wawakilishi.
Hata hivyo, alisema mafanikio hayo yamekuja kutokana na mashirikiano ya pamoja kati ya madiwani, watendaji na halmashauri katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.
“Kiutendaji halmashauri imekusanya asilimia 62 ambazo zinakwenda kwenye maendeleo ya halmashauri ikiwemo miradi inayotekelezwa na halmashauri baada ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka”, alisema.
Aidha alisema katika kipindi cha miaka mitano halmashauri ilitekeleza miradi 82 ambapo awamu ya kwanza ilitekeleza miradi 51 na awamu ya pili ilitekeleza miradi 31.
Makame alisema miradi saba iko katika hatua za mwisho ambayo nayo inawalenga wananchi kuwapatia huduma.
Mkurugenzi huyo, aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa maji safi na salama, miradi ya ukarabati wa vituo vya afya, kilimo, ujenzi wa barabara za ndani na mengineyo.
Hata hivyo alisema lengo la halmashauri ni kuhakikisha miradi yote inamalizika kwa wakati ifikapo Juni 30 mwaka huu ambapo miradi saba ndio inamalizia katika awamu hii.
MRADI WA UKUMBI WA MIKUTANO
Katika ziara aliyoifanya hivi karibuni akiongozana na watendaji wake, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Makame Mwadini Silima, alisema ujenzi wa Ukumbi wa kufanyia mitihani Bumbwini Misufini ni moja ya mradi unaotekelezwa na halmashauri hiyo ili kurahisisha upatikanaji mzuri wa huduma kwa wanafunzi wa skuli hiyo.
Alifahamisha kuwa mradi huo ulipitishwa na wananchi kupitia wadi baada ya kutoa maoni yao ya kujengewa ukumbi huo, hivyo halmashauri ilitekeleza mradi huo kwa asilimia 90.
“Ukumbi huu utakapomalizika utatumika kwa shughuli zamkoa mzima ikiwemo mikutano ya kijamii na mengineyo ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi milioni 114 ambapo kwa sasa ujenzi huo upo asilimia 90”, alisema.
Akifafanua zaidi alisema kuwa kati ya fedha hizo asilimia 90 ni mchango wa halmashauri na huku asilimia 10 ni mchango wa Mbunge wa Jimbo hilo pamoja na Wizara ya elimu ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Alisema ukumbi huo sio tu utatumika kwa ajili ya kufanyia mitihani kwa wanafunzi wa skuli hiyo bali pia utatumika kwa shughuli za kijamii ikiwemo mikutano.
“Huu mradi sisi ni watekelezaji tu na wananchi ndio wenyewe kwani ndio waliopendekeza kujengewa ukumbi na ndio maana tukaamua kufanya hivyo kwa maslahi ya pande zote mbili”, alisema.
Makame alitaka mara baada ya kukamilika na kutumika kuutunza vyema ukumbi huo ili uweze kudumu.
Nae Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya hiyo ambae pia ni Diwani wa Wadi ya Bumbwini Misufini, Ame Simai Daima, aliishukuru halmashauri hiyo kwa utekelezaji wa mradi huo.
MRADI WA BARABARA YA NDANI MANGAPWANI.
Akizungumzia kuhusiana na mradi wa barabara ya ndani ya kijiji cha Mangapwani, Mkurugenzi Makame alisema ujenzi wa barabara hiyo ni moja ya miradi iliyopendekezwa na wananchi na kutekelezwa na halmashauri ambapo hadi sasa umefikia asilimia 98 ya ujenzi wake.
“Hadi kukamilika kwake mradi huu utagharimu shilingi milioni 30 ambapo pamoja na mambo mengine lakini umewekewa miundombinu ya maji machafu ili uweze kudumu kwa muda mrefu”, alisema.
Mkurugenzi Makame alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutamaliza kilio cha wafanyabiashara wa madagaa Mangapwani ambao ndio walengwa wakubwa wanaotumia barabara hiyo.
MRADI WA UKARABATI WA KITUO CHA AFYA KITOPE
Kwa upande wa ukarabati wa kituo cha Afya Mkurugenzi huyo, alisema wametumia shilingi milioni 20 kufanya ukarabati wa kituo cha afya Kitope.
“Kwa kuwa kituo hiki kinatumiwa na watu wengi kwenye halmashauri hii tumeamua kukiboresha ili kuona kwamba kinatoa huduma nzuri kwa jamii”, alisema.
Nao wafanyakazi wa kituo hicho waliishukuru halmashari hiyo kwa maamuzi ya kufanya ukarabati kituo hicho na kuomba kumaliziwa ujenzi wa kisima ili na huduma ya maji ipatikane kituoni hapo.
“Tunalazimika kupata huduma hii kutoka kisima kinachotumiwa na wananchi wa eneo la karibu na kituo hicho hivyo kama halmashauri itakamilisha uchimbaji wa kisima tutaondokana na usumbufu tunaoupata sasa pamoja na wagonjwa wetu tunaowahudumia”, alisema mmoja wa wafanyakazi wa kituo hicho.
MRADI WA KITUO CHA AFYA MAHONDA.
Kwa upande wa kituo cha afya cha Mahonda, Mkurugenzi huyo alisema mradi huo umegharimu shilingi milioni 22 kwa kununulia vifaa mbalimbali vya matibabu kituoni hapo.
Mkurugenzi huyo, alisema halmashauri imeamua kutekeleza mradi huo baada ya kupokea mapendekezo ya wananchi kupitia madiwani juu ya mradi huo.
Mganga mkuu wa kituo hicho, Iddi Mohamed Mahmoud, alisema kuwepo kwa huduma hiyo kituoni hapo itarahisisha upatikanaji wa huduma za kinywa na meno ambapo hapo kabla hazikupatikana.
MIRADI YA BARABARA ZA NDANI WADI ZA DONGE VIJIBWENI, MKATALENI
Kuhusina na miradi ya barabara za ndani katika vijiji vya Doinge na Mkataleni, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo alisema miradi hiyo tayari inaendelea na iko katika hatua nzuri huku fedha zake zikitokana na mfuko wa halmashauri kwa asilimia 90.
“Barabara hizo zitatumia shilingi milioni 215 na zina urefu wa kilomita tatu na asilimia 85 zitajengwa kwa nguvu za halmashauri na asilimia 15 kutoka kwenye mfuko wa Jimbo ambao utatolewa na Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Donde.
Makame alisema kujengwa kwa barabara hizo kutaondosha usumbufu waliokuwa wakiupata wananchi wa kusafirisha mazao yao kutoka maeneo ya ndani hadi barabarani huku kukiwa na masafa marefu.
UJENZI NA UKARABATI WA KITUO CHA AFYA DONGE VIJIBWENI
Sambamba na miradi hiyo, lakini Mkurugenzi Makame alisema kituo hicho ni nguvu za viongozi wa jimbo pamoja na halmashauri jambo ambalo limerudisha miradi hiyo katika jamii.
Alisema kituo hicho kitakapokamilika kitatoa huduma bora kwa wananchi wa jimbo hilo ambao ndio walengwa wakubwa watakaokitumia kituo hicho.
MWENENDO WA UKUSANYAJI WA MAPATO
Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato kiujumla wake, Mkurugenzi Makame alisema mwenendo wa ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka mwaka 2015-2016 hadi 2020.
“Katika ukusanyaji huo hatutegemei sana mapato yatokanayo na mchanga kwa sasa na pia tumeongeza siku za kukusanya mapato, hakuna siku ambayo halmashauri haikusanyi mapato”, alisema.
Akitoa ufafanuzi alisema mwaka wa kwanza halmashauri ilijipangia kukusanya shilingi milioni 5.3. na kufanikiwa kukusanya shilingi milioni 4,3. sawa na makusanyo ya asilimia 81 ya lengo walilojiwekea.
Mwaka 2016-2017 walijipangia kukusanya zaidi ya shilingi milioni 5.6. na kukusanya shilingi milioni 6.7. sawa na asilimia 120 ya lengo.
“Kwa mwaka 2017-2018 tulijipangia kukusanya shilingi milioni 5.8. na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 1.2. sawa na asilimia 213 ya lengo tulilojipangia, inaonesha Dhahiri kuwa mapato yameongezeka maradufu”, alisema.
Aidha alisema kwa mwaka 2018-2019 halmashauri ilitegemea kukusanya shilingi bilioni 1. 6 na kukusanya shilingi bilioni 1.4. sawa na asilimia 88 ya lengo tulilojiwekea ingawa haikufika.
Sambamba na hilo, Mkurugenzi huyo alisema kwa mwaka 2019-2020 halmashari ilikusanya shilingi bilioni 2. 11 na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 1.4. sawa na asilimia 70.
Alisema kiwango hicho kilipungua kutokana na kujitokeza kwa janga la ugonjwa wa corona ambalo kwa kiasi kikubwa liliathiri ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hiyo.