PARIS, UFARANSA

KUMESHUHUDIWA ghadhabu miongoni mwa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja huo kuhusiana na virusi vya corona kukosa suluhisho.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwashambulia viongozi wa Uholanzi na Austria na kutishia kutoka kwenye mkutano huo.

Kumekuwa na hali ya kupoteza matumaini kwa siku tatu wakati ambapo viongozi 27 wa Umoja huo wakijadiliana kuhusiana na ukubwa na jinsi ya kugawanya hadi yuro bilioni 750 kama mikopo kwa nchi zilizoathirika  na virusi vya corona ili kunusuru uchumi wao.

Muungano wa nchi zinazotaka udhibiti wa utoaji wa pesa hizo ukiongozwa na Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte na Kansela wa Austria Sebastian Kurz, ulikuwa ukipinga hatua ya kutolewa kwa pesa hizo kama mikopo ambayo haitolipwa.

Taarifa zinaeleza kuwa wakati mmoja katika mkutano huo Macron alionekana kuipiga meza kwa mkono kwa hasira na kumshambulia Kurz kwa kuondoka chumba cha majadiliano ili ajibu simu na alimshutumu Rutte akisema anafanya vile alivyofanya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza David Cameron ambaye mpango wake ulimtumbukia nyongo.